
WAKATI zikibaki mechi sita kuhitimisha msimu huu wa Ligi ya Championship, washambuliaji wa Mbeya City wamekuwa tishio kufunga mabao matatu kwa mechi moja yaani ‘hat-trick’, tofauti na nyota wengine kutoka timu mbalimbali zinazoshiriki.
Hadi sasa jumla ya hat trick nne zimefungwa ikibakisha moja tu kuifikia rekodi ya msimu uliopita zilipofungwa tano huku Mbeya City ikitoa nyota wawili, wakati kwa upande wa Geita Gold na Mbeya Kwanza zikitoa mchezaji mmoja kwa kila upande.
Nyota wa kwanza kufunga hat trick ni Faraji Kilaza Mazoea wa Mbeya City aliyeifungia timu hiyo katika ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya Polisi Tanzania aliyowahi kuichezea, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Desemba 13, 2024.
Andrew Simchimba wa Geita Gold akawa ni mchezaji wa pili msimu huu baada ya kufunga pia hat trick wakati kikosi hicho kikiitandika Transit Camp kwa mabao 4-0, kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita, Februari 10, 2025.
Mwingine ni Oscar Tarimo aliyeifungia Mbeya Kwanza aliyojiunga nayo dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea Polisi Tanzania, wakati kikosi hicho chenye maskani yake mjini Mtwara kikiichapa Biashara United mabao 5-0, Februari 23, 2025.
Mshambuliaji wa mwisho ni William Thobias aliyeifungia Mbeya City katika ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya Kiluvya United, mechi kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Machi 17.