
SIKU moja baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania masjala kuu ya Dodoma kuamuru kuitwa kortini wachezaji watatu wa Singida Black Stars, ili kujibu madai dhidi yao katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Wakili Peter Madeleka, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imethibitisha kwamba nyota hao wamesajiliwa kama wachezaji wa ndani.
Amri ya mahakama ilitolewa jana baada ya wachezaji hao Emmanuel Keyekeh, raia wa Ghana, Josephat Bada (Ivory Coast) na Mohamed Damaro Camara (Guinea) kutotokea mahakamani katika kesi dhidi yao ilipotajwa mbele ya Jaji Evaristo Longopa, wanakoshtakiwa kwa kupata uraia wa Tanzania kinyume cha utaratibu.
Baada ya shauri hilo kutajwa na wachezaji hao kutotokea, Jaji Longopa aliagiza waitwe tena kwa wito wa mahakama (samansi) na wawe wamejibu madai yaliyopo katika hati ya madai kabla ya Machi 4, 2025.
Hata hivyo, huku nyuma tayari wachezaji hao wameingizwa kwenye mfumo wa soka kama raia wa Tanzania.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Said Soud alithibitisha kuwa wachezaji hao wamesajiliwa kama raia wa ndani ya nchi.
“Mamlaka husika imetoa kibari cha kuwapa uraia wachezaji hao, sisi ni nani tushindwe kuifuata na kuwasajili wachezaji hao kutokana na uraia waliopewa. Ni kweli ni wachezaji wa ndani tangu mamlaka hiyo ilipotoa taarifa,” alisema.
Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almas Kasongo alisema hawezi kulizungumzia kwa kina suala hilo, lakini wanaheshimu uamuzi wa taasisi yenye dhamana ya uraia kuwapa uraia wa Tanzania wachezaji hao.
“Hilo siwezi nikalizungumzia kwa mapana na marefu, lakini kitu ambacho naweza kukielezea kwa uhakika taasisi yenye dhamana ya uraia imetoa taarifa kwamba wachezaji wamepewa uraia. Naamini chombo kutoa taarifa hiyo siwezi kuwa na neno zaidi ya kukiamini chombo cha Serikali kwa uamuzi walioutoa,” alisema na kuongeza:
“Kurugenzi ya Mashindano chini ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, usajili ukishakamilika sisi (Bodi ya Ligi) ndio tunaletewa huku kwa ajili ya matumizi. Kwangu nafikiri watu wa Idara ya Mashindano ndio wanaweza kutoa ufafanuzi.”
Kasongo alisema kama mtendaji mkuu ni anaamini taarifa ya mamlaka yenye dhamana ya mambo ya uraia kutoa taarifa kuutaarifu umma kwamba wachezaji hao wamekuwa raia, kwa upande wake hana kipingamizi.
“Nina wajibu wa kukiamini chombo cha serikali kwamba wamefuatilia mchakato kwa usahihi na kutoa uraia kwa wachezaji hao. Lakini suala la kuwa raia na mambo ya usajili ni vitu viwili tofauti, usajili una mahitaji yake na uraia una mahitaji yake.
“Kuwa raia haikufanyi uweze kusajiliwa timu fulani kwa sababu usajili una mahitaji yake. Ukikamilisha, basi usajili utakuwa umekamilika. Ni mahitaji gani sasa wanatakiwa wakamilishe na kupeleka kwenye Idara ya Mashindano ambao wanasimamia usajili ili kupata uhakika.”
Kasongo alisema wachezaji wote wenye sifa za kusajiliwa wamefanya hivyo na wanacheza, na kama kutakuwa na changamoto za kiusajili zinakuwa za kawaida ambazo ni kwa ajili ya kutimiza matakwa yanayotakiwa.
Taarifa za raia hao wa kigeni kupewa uraia zilianza kujadiliwa katika mitandao ya kijamii na baadaye kuchapishwa katika vyombo vya habari ndipo Januari 23, 2025, Idara ya Uhamiaji ikajitokeza hadharani na kuthibitisha ukweli wa jambo hilo.
Katika taarifa kwa umma iliyotiwa saini na Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji (SSI), Paul Msele ilisema wachezaji hao waliomba na kupewa uraia chini ya vifungu namba 9 na 23 vya Sheria ya uraia wa Tanzania, sura ya 357.
WACHEZAJI WA KIGENI SINGIDA BS
Amas Obasogie
Anthony Tra Bi Tra
Victorien Adebayor
Jonathan Sowah
Frank Assinki
Ande Cirille
Serge Pokou
Elvis Rupia
Marouf Tchakei
Ibrahim Imoro
Hernest Malonga
Morice Chukwu