
Kutoka na kifo cha nguli wa muziki wa dansi marehemu Boniface Kikumbi ‘King Kikii’.Baadhi ya wasanii wakongwe wa muziki huo nchini wameiambia Mwananchi namna walivyoguswa na kifo hicho.
Nguza Viking ‘Babu Seya’
“King Kikii nimefanya naye kazi na sio kazi tu bali ni kama ndugu yangu maana ndio alinipokea kwenye bendi ya Maquis du Zaire, nyumbani kwetu alikuwa anafahamiana na wazazi wangu na ndugu zangu kwahiyo kwangu ni kama kaka.
“Wakati anaumwa nilikuwa nawasaliana naye mara kwa mara, kipindi cha mwisho cha uhai wake kuna mambo ya ndani mengi tulikuwa tunaongea kwa sababu mimi ni miongoni mwa watu alikuwa anaelewana nao sana, hata itokee shida gani nilikuwa nikiongea naye ananielewa” amesema Babu Seya .
Babu Seya akiwa mmoja wa wasanii wa muziki wa Dansi nchini, amesema King Kikii aliipenda Tanzania mpaka kufukia hatua ya kubadilisha uraia wake, kutoka wa Kongo kuwa Mtanzania.
“King Kiki aliomba uraia kuwa Mtanzania kwa sababu aliingia nchini miaka ya 1977 na alishi miaka mingi kwahiyo akaomba uraia” amesema Babu Seya
Zahir Zorro
Naye mkongwe wa muziki wa dance nchini Zahir Zorro ameiambia Mwananchi alikuwa akifanya nae mazoezi.
“Ni msiba mkubwa sana alikuwa mwanamuziki bora sana wa Rhumba, ameweka heshima kubwa sana kwenye muziki wa Tanzania na aliipenda Tanzania maana ameishi hapa tangu mwaka ya 1970, na niliwahi kufanya kazi kwenye bendi ya Samburuma ila sikubahatika kurekodi naye wimbo wowote.
“Tangu miaka ya 1970 yupo hapa Tanzania na alikaa miaka mitano kisha akaondoka na bendi ya Afro Band wakazunguka wakaenda Zambia wakaibadilisha jina wakajiita Safari
Coy, mwaka 1978 akarudi Tanzania akaingia bendi ya Maquis du Zaire akaubadilisha sana muziki watu wakapenda kuusikiliza na kucheza akawa anaimba vizuri kiswahili akatoka wakaanzisha Masantula watu wakaendelea kumpenda, “amesema Mzee Zollo
Kwa upande wake Mc Garab kupitia ukurasa wake wa Instagram amechapisha salamu za pole kwa familia ya marehemu
“Legend King KiKii is gone, Pole sana @jessicakikumbi umempambania sana mzee. Pole kwa familia na wapenda burudani, hususan muziki wa dansi. Vita amevipiga na mwendo ameumaliza. Tutaendelea kuenzi kazi zako.#RIPKingKikii,”ameandika Garab
Naye Haji Manara kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika,
“Legend kaondoka.Mwamba King Kikii hatupo nae tena duniani. Mbele yake na Sisi tunafuata. Nowdays kila ukiamka unakutana na taarifa za misiba tena ya watu tunaowajua,Israel keshasogea jirani yetu, tuendelee kukumbushana kumrejea Muumba wetu,”ameandika Haji
Aidha Steve Mengele ‘Steve Nyerere’ kupitia ukurasa wake wa Instagram ameeleza kuwa nyimbo za King Kikii zitabaki kama alama ya taifa.
“Utunzi na ubunifu ni kipaji alicho kupa Mungu.History umeitendea haki miaka na miaka na ndomana mpaka leo kuna kizazi kinakujua kwa Kitambaa Cheupe. Nyimbo zako zinamsimamisha mtu yeyote yule kwenye kiti aweze kucheza.Hakuna nyimbo yako hata 1 iliyowahi kuzoeleka kwenye Masikio ya Watanzania bali unaposikia kwa mara ya kwanza unaamini ni kibao kimpya.
“Nyimbo hizo hizo umewambia mababu zetu kizazi cha kati na kizazi cha leo wamesikiliza na kucheza pia,umelala tangulia tutaishi maisha yako ya unyenyekevu.Nidhamu maarifa na juhudi. Mchango wako kwenye maisha ya watu ni mkubwa sana hasa pale ulipoamua kuwapa ajira wazee wenzako kupitia bendi yako.Tutaonana Baadaye Pumzika kwa Amani,”ameandika Steve
King Kikii amefariki usiku wa kuamkia leo Novemba 15, 2024 nyumbani kwake Mtoni Kwa Aziz Ally jijini Dar es Salaam.