Kifo cha bondia mstaafu wa ngumi za uzito wa juu duniani, George Foreman kimeonekana kugusa mastaa mbalimbali wa michezo ambao wameipa pole familia yake huku wakionyeshwa kuguswa nacho.
Foreman amefariki dunia jana Ijumaa, Machi 21, 2025 huko Texas, Marekani akiwa na umri wa miaka 76 na sababu ya kifo chake bado haijawekwa wazi.
Mastaa hao wametumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kuonyesha kuguswa kwao na kifo hicho huku wakitoa pole kwa familia yake.

“Salamu za rambirambi kwa familia ya George Foreman. Mchango wake kwenye ngumi na zaidi hautosahaulika,” alisema Mike Tyson.
Mshindi mara sita wa taji la Ligi Kuu ya Kikapu Marekani (NBA), Scottie Pippen ameandika,”Pumzika kwa amani George Foreman. Heshima yako bado inaishi bingwa.”
Nyota wa zamani wa mpira wa kikapu, Magic Johnso amesema kuwa George Foreman alimfanya apende mchezo wa ngumi.

“Nina huzuni kusikia taarifa za kifo cha mmoja wa mashujaa wangu wa ngumi, George Foreman. Nimehudhuria mapambano yake mengi. Alikuwa ni msanii wa kuangusha watu kwa KO katika ulingo na ilikuwa jambo zuri kufahamiana naye sio tu kama bondia bali kama binadamu.
“Baada ya kuacha ulingo, aligeuka kuwa mfanyabiashara wa kipekee. Niliwahi kununua nyama choma ya kwanza katika. Nitakuwa naiombea familia yake katika kipindi hiki,” amesema Johnson.
Muigizaji wa filamu za vichekesho, Loni Love amesema,” Bingwa ameenda. Mkubwa katika maisha kwenye njia nyingi zaidi ya moja. George Foreman aliteka nyoyo na hisia za mashabiki wa michezo. Bingwa mara mbili wa ngumi za uzito wa juu duniani, muwekezaji, mtunzi na muhubiri, George Foreman amefariki Ijumaa akiwa na umri wa miaka 76.”