Dar es Salaam. Jana Februari 19,2025 mwanamitindo Hamisa Mobetto na mumewe Aziz Ki walikuwa wakimalizia sherehe yao ya harusi waliyofunga Februari 16,2025.
Kutokana na ukubwa wa sherehe hiyo, iliwafanya mastaa mbalimbali waliohudhuria kuvunja makabati na kutokea wakiwa na mionekano bomba iliyozua mijadala kwenye mitandao ya kijamii.
Kati ya mastaa waliohudhuria sherehe hiyo ni mastaa, Marioo na Paula, Lulu Diva, Wema Sepetu, Jackline Wolper, Nandy, Haji Manara na mke wake Zaylissa na wengineo. Pigo zao zilikuwa hivi.
Aziz Ki na Hamisa Mobetto
Ukianza kwa wenye shughuli wenyewe wameutendea haki usiku wao, ambao ulikuwa wa kipekee kwa kubadilisha nguo mara mbili huku awamu ya kwanza wakivaa mavazi yenye rangi nyeupe na ya pili yakiwa ya blue mpauko.
Kutokana na mavazi hayo, wengi katika mitandao ya kijamii wamekuwa wakisifia zaidi vazi la pili wakidai halikuwa na mambo mengi.

Jackline Wolper
Moja ya mastaa ambao wamekuwa wakijadiliwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii ni mwigizaji na mfanyabiashara Wolper ‘Mama P’. Ni kutokana na vazi alilotupia huku wengi wakinanga pochi yake kubwa ambayo amekuwa akionekana nayo mara kadhaa kwenye matukio mbalimbali.

Maoni mengi yamekuwa yakiponda na mengine kupongeza mwonekano wake. “Watu wamekariri kuvaa uchi ndiyo kupendeza, hata pochi ni style yake ya nitoke vipi ndio maana anaongelewa maana katoka kipekee”, “Huyu dada kajiheshimu na kajielewa,” hizo ni baadi ya komenti za mashabiki
Aidha wakati akiwa kwenye zuria jekundu katika usiku huo, aliweka wazi kuwa ameamua kuwa na mwonekano tofauti ili atakapochukiza au kupendeza awe wa kipekee.
Wema Sepatu
Wema naye alikuwa mmoja wa mastaa ambao walihudhuria katika usiku huo, ambao ulikuwa mahususi kwa rafiki yake na mtu wake wa karibu kwa muda mrefu. Wema alivalia vazi flani linaloendana na shela jambo ambalo lilizua mjadala huku wadau na mashabiki wakieleza kuwa hakupaswa kuvaa hivyo.

“Jamani White dress tena shela kwa harusi ya mwenzio kheee,”, “Hii sio nguo ya kwenda nayo kwenye harusi ya mwenzio kapania halafu kaharibu, mwingine akiandika “Kuanzia kichwani hadi tuponi kapendeza ila huku chini hapana” maoni kutoka kwa wadau na mashabiki katika mitandao ya kijamii
Mr & Mrs Manara (Haji Manara na Zaylissa)
Kama ilivyo kawaida ya wanandoa hawa ambao wametimiza mwaka mmoja wa ndoa yao wiki chache zilizopita. Kupendeza katika sherehe mbalimbali wanazoalikwa, katika usiku huu wa Hamisa na Aziz wawili hao walivalia mavazi ambayo yamevutia baadhi mashabiki huku wengi wakiwananga kwa mtoko wao huo.
“Kwenye harusi yenu mmeshindwa kupendeza mnafosi mpendeze kwenye harusi ya watu, lakini imeshindikana mmejisahau kama hata iweje uwezi kumzidi Hamisa kwa kupendeza, mmeonekana washamba tuu”,

Huku nyingine ikisema “Watu wa Insta sasa utasikia hamjapendeza acha niongee ukweli Bugat unazidi kuonyesha ukubwa wako kila panapokucha umeionesha dunia kuwa ukioa mwanamke anayejielewa huwezi kuwaza kumuongezea mwenzake mnazidi kung’aa kila kukicha mlipendeza sana hongera kwako,”
Mama wa bibi harusi (Shufaa Lutigunga)
Licha ya kupokea maoni tofauti tofauti katika mitandao ya kijamii yakieleza kuwa alipokuwa akiingia ukumbini alikuwa amenuna. Lakini kwenye upande wa mavazi mama wa bibi harusi hakuwa na mambo mengi, huku wengi wakimsifia kutokana na mwonekano pamoja na rangi aliyoichagua.

Wachezaji wa Yanga
Moja ya jambo lililowavutia watu wengi katika usiku huo, ni wachezaji wa Yanga wakiongozwa na msemaji wao Ally Kamwe, Kibabage, Kibwana, Mishery, Job, Mwanamnyeto na wengineo wakiwa katika mstari wa mbele kuhakikisha Aziz Ki anafurahia usiku huo.

Kwa upande wa mavazi klabu ya Yanga imeupiga mwingi kutokana na mwonekano waliotoka nao kuwavutia mashabiki.
Mbali na mastaa hao kuwaka na kupata maoni tofauti, katika mitandao ya kijamii wapo mastaa wengine ambalo walitenda haki ni pamoja na Mwijaku na mke wake, Posh Queen, Bi Star, Nandy, Yammy, Juma Lokole, Feza Tessy na wengineo