Mastaa wakongwe Simba wamtaka Mukwala

Mastaa wa zamani wa Simba, wanatamani Kocha wa timu hiyo, Fadlu Davis akamuanzia raia wa Steven Mukwala kwenye kikosi cha kwanza kitakachowavaa Al Masry Jumatano jioni kwenye Uwanja wa Mkapa.

Simba inahitaji ushindi wa mabao 3-0 kwa bila ili kusonga mbele kwenye hatua na nusu fainali ya Kombe la Shirikisho na kuweka rekodi mpya baada ya kufuzu robo maranyingi.

Mastaa hao wanaamini kwamba Mukwala ana uwezo wa kutumia nafasi chache na akaipa Simba matokeo magumu wanayohitaji kuliko Lionel Arteba anayetumika maranyingi.

Kocha Boniface Pawasa ambaye ni beki wa zamani wa Simba licha ya kuwataka wachezaji wa timu hiyo kuwa makini na dakika 20 za kwanza, amemtaka kocha Fadlu kuchagua kuanza na Mukwala ambaye kaliba ya uchezaji wake utasaidia kuwatawanya mabeki wa Al Masry.

Pawasa aliongeza kuwa Fadlu kama ataendelea kumuamini Ateba itawapa faida mabeki wa  Waarabu hao ambao watakuwa na wakati mzuri  wa kumdhibiti kwa kuwa hupenda kutulia eneo moja.

“Mimi nadhani angeanza na Mukwala unajua Mukwala anapenda kuhangaika kule na huku, aina ya uchezaji wake utawafanya mabeki kutawanyika pale kati.

“Kutawanyika kwao kutatoa nafasi kwa kina Kibu, Mpanzu na hata Ahoua kufanya mambo makubwa kwenye mashambulizi kuliko kumtumia Ateba ambaye anapenda kutulia eneo moja, mabeki wengi wanapenda kumkaba mtu kama Ateba wana uhakika watamtuliza kirahisi.

“Simba inaweza kushinda lakini lazima iwe makini na dakika 20 za kwanza, Waarabu watakuja kwa nguvu sana na kwa hesabu kali wakifanya makosa ya kushambulia vibaya wanaweza kupata wakati mgumu,”alisema Pawasa ambaye kitaaluma amesomea ukocha.

Naye staa wa zamani wa Simba Zamoyoni Mogela alisema wachezaji wanatakiwa kucheza kwa akili kubwa kutafuta mabao lakini pia kuweka ulinzi sawasawa kwa kuwa wapinzani wao hawatakuja na akili ya kujilinda peke yake.

“Kama ataanza Ateba au Mukwala wanatakiwa kutambua kwamba mashabiki wanakuja uwanjani kuona kazi yao bora kwahiyo wanatakiwa kutulia na kufanya mambo, kwa ujumla wanatakiwa wachezaji wote kucheza kwa umakini kuanzia nyuma mpaka mbele,”alisema Mogella.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba na kocha Abdallah Kibaden ‘King’ alisema; “inawezekana kocha anataka kumtumia Ateba lakini ninachoweza kumshauri azungumze na wasaidizi wake kwenye timu kama watamwambia aanze na Mukwala badala ya Ateba basi ajaribu kuwasikiliza kwa kuwa watakuwa na kitu wameona kupitia wachezaji hao wawili.

“Kwangu mimi naamini Simba bado ina nafasi ya kufanya mambo mazuri kwa kutengeneza ushindi mzuri kitu muhimu wachezaji wajitambue na kufanyiana wepesi ili wapate matokeo mazuri wanayoyataka.”

Kwa upande wa kiungo Dua Said alisema; “Ukitazama namna Ateba alivyocheza mchezo wa kwanza hata ukiniuliza mimi nitakwambia ni bora aanze Mukwala lakini shida yangu ni tofauti kidogo. Inawezekana tunamuona Ateba tatizo lakini tuwaangalie wale viungo wanaocheza kumzunguka, Ahoua (Jean Charles) na kina Mpanzu (Elie) na Kibu (Denis) ukiona namna wanavyocheza wanampa wakati mgumu Ateba wanamuacha mbali sana lakini pia waache ubinafsi.”

HESABU ZA ZILIVYO

Ni kupata mabao 3-0 dhidi ya Al Masry ili kufukia ushindi wa Waarabu hao waliupata kwenye mchezo wa kwanza kule Suez wa mabao 2-0.

Simba inatakiwa kujipanga sawasawa dhidi ya Al Masry ambayo takwimu zinaonyesha sio timu rahisi kufungika kwa zaidi ya mabao mawili. Msimu huu kwenye mechi tatu za makundi ugenini ilipoteza mchezo mmoja dhidi ya ndugu zao Zamalek kwa bao 1-0 lakini ikatoa sare mbili ya bao 1-1 dhidi ya Enyimba ya Nigeria na Black Bulls ya Msumbiji.

Matokeo hayo yanaonyesha kwamba wakati Simba inataka mabao matatu isiruhusu bao kutokana na wageni wao wameshafunga mara mbili kwenye viwanja vya ugenini.

Masry ikiwa ugenini inajaza viungo wengi katikati ukiwa na lengo la kutengeneza wepesi kucheza mashambulizi ya haraka.

KILA ASISTI MIL 2.5

Kama mipango itabaki vilevile, Mwanaspoti linajua MO Dewji na jopo lake la viongozi wameweka mezani mzigo wa sh 500 milioni kama bonasi kwa wachezaji wake endapo watafuzu kwenda nusu fainali.

Kama haitoshi, matajiri wengine wamejipanga na kuwatangazia wachezaji kwamba kila asisti itakayotengeneza bao kwenye ushindi huo na wakafuzu itanunuliwa kwa sh 2.5 milioni lakini pia mfungaji wa bao naye atapata kiasi kama hicho.

Hesabu zao hapa ni kutaka kuona makosa ya kunyimana pasi kama ambavyo ilionekana kwenye mchezo wa kwanza hayajirudii kwenye mechi ya leo.

MABAO, ULINZI

Kocha Fadlu kwenye mazoezi ya juzi pale Uwanja wa Mkapa, alionekana kuwa mkali kwa wachezaji wake kuhakikisha kikosi hicho kinatengeneza nafasi na wanazitumia kwa wingi lakini pia alikuwa akikomaa na kuhakikisha eneo la kiungo cha chini viungo wake Yusuf Kagoma,Fabrice Ngoma na mabeki wa kati, wanakuwa kwenye ubora wa kuzima mashambulizi ya wapinzani.

Kule kwenye kufunga hata mabosi wa timu hiyo waliohudhuria mazoezi walionyesha kuridhishwa namna washambuliaji Lionel Ateba, Steven Mukwala na viungo wengine washambuliaji Elie Mpanzu,Kibu Denis na Jean Charles Ahoua walivyokuwa wanacheza kwa ushirikiano na kufunga mabao.

Simba inatakiwa kujipanga sawasawa na kuishi kwa akili kubwa na mwamuzi wa mchezo huo Djindo Louis Houngnandande kutoka Benin ambaye hapa nchini amewahi kuamua mechi za watani wao Yanga na zote mbili wakapotea kwa vipigo ikipigwa 1-0 ugenini dhidi ya Al Ahly lakini pia alikuwa mezani wakati Yanga ikilala kwa mabao 2-0 dhidi ya Rivers United mechi zote za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Houngnandande hana ajizi katika kumwaga kadi za njano kwenye mechi ambazo anaziamua ambapo kadi zake nyekundu mbili alizozitoa zilitokana na mchezaji kupata kadi ya pili ya njano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *