Mastaa Twiga Stars waitisha Guinea Ikweta

Dar es Salaam. Wakati zikibaki siku nne kabla ya mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcon) 2026 dhidi ya Guinea Ikweta, nyota wa timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ wametamba kupata ushindi nyumbani.

Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo utachezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Alhamisi, Februari 20 mwaka huu na zitarudiana jijini Malabo, Guinea Ikweta, Februari 26 mwaka huu.

Mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Stumai Abdallah alisema wanaamini watapata ushindi dhidi ya Guinea Ikweta.

“Sisi ni timu bora hatuna hofu ya kukutana na timu yoyote, hivyo kuhusu mechi yetu ya tarehe 20 tupo tayari kuwakabili Guinea Ikweta,” alisema Stumai.

Nyota mwingine wa Twiga Stars, Aisha Mnunka alisema kuwa

“Sisi tunajiamini, kitu kikubwa ambacho kocha amekuwa akitusisitiza kuelekea mchezo wetu dhidi ya Equtorial Guinea tarehe 20, ni kujitoa na kupambana kizalendo,” alisema Mnunka.

Mshindi wa mechi mbili baina ya Twiga Stars na Guinea atakutana na timu itakayofuzu baina ya Uganda na Ethiopia katika raundi ya kwanza na ya mwisho ya mashindano ya kufuzu ambapo itakayopenya hapo itatinga fainali za Wafcon 2026 zitakazofanyika Morocco.

Ikiwa Twiga Stars itafuzu fainali za Wafcon 2026, itaweka rekodi yake ya kushiriki fainali hizo kwa mara ya pili mfululizo, ya kwanza ikiwa ni za 2024 zinazochezwa mwaka huu Morocco.