Mastaa Simba wakwepa mtego CAF

KITENDO cha mastaa wa Simba SC kucheza kwa nidhamu kubwa dhidi ya Al Masry katika michezo miwili ya hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kimewaepusha na mtego wa CAF unaoweza kuwaengua katika fainali iwapo wataitoa Stellenbosch FC ya Afrika Kusini.

Katika mechi hizo mbili dhidi ya Al Masry, ile ya kwanza iliyochezwa Port Said, Misri, Simba walifungwa 2-0, lakini wakapindua matokeo kwa ushindi wa mabao 2-0 nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kabla ya kushinda kwa mikwaju ya penalti 4-1 na kufuzu nusu fainali.

Mchezaji pekee wa kikosi hicho aliyeonyeshwa kadi ya njano katika hatua hiyo ya robo fainali ni beki wa kati, Chamou Karaboue, katika mchezo wa kwanza ugenini. 

Kanuni za CAF, Ibara ya 38.1 inasema: “Mchezaji atakayepokea kadi tatu za njano katika mechi tatu tofauti za mashindano atafungiwa moja kwa moja mechi inayofuata ya mashindano hayo.”

Simba ambao kwa sasa wanakosa huduma ya beki wao tegemeo Che Fondoh Malone, aliyepata majeraha wiki chache zilizopita, hawana nafasi ya kupoteza mchezaji mwingine wa kikosi cha kwanza kwa adhabu ya kadi za njano tatu. Hali hii inamfanya Karaboue kuwa kwenye presha ya kuepuka kadi kwa ajili ya fainali.

Mbali na Karaboue, mastaa wengine wa Simba waliokuwa kwenye hatihati ya kupata kadi katika mechi za robo fainali ambao ni Moussa Camara, Kibu Denis, Yusuph Kagoma, Leonel Ateba, Elie Mpanzu na Che Fondoh Malone, walicheza kwa utulivu mkubwa, jambo ambalo linaonyesha namna benchi la ufundi la Fadlu lilivyoweka msisitizo kwenye nidhamu ya kiuchezaji.

CAF imeweka wazi kuwa kadi za njano ambazo hazijasababisha kuzuiwa kucheza mchezo unaofuata zinafutwa mwisho wa hatua ya makundi. Hii ina maana kuwa mastaa wa Simba waliopata kadi za njano hatua ya makundi waliingia robo fainali wakiwa safi kutokana na kadi zao hizo mojamoja kufutwa kabla ya Karaboue kupata ya njano moja hatua ya robo fainali ambayo anaendelea kuwa nayo hadi mwisho wa mashindano.

Endapo ataonyeshwa kadi mbili zingine za njano katika mechi mbili za nusu fainali, basi hatacheza fainali kama Simba itafuzu, pia ikitokea mchezaji mwingine akapata kadi tatu za njano katika mechi mbili za nusu fainali na ile ya fainali ya kwanza kama Simba itafuzu, basi hatacheza mechi ya mwisho.

Hata hivyo, kwa mchezaji atakayepata kadi nyekundu moja kwa moja katika mechi yoyote, adhabu yake ni kuzuiwa kucheza mechi inayofuata, bila kujali hatua ya mashindano.

Pia, CAF ina mamlaka ya kuongeza adhabu zaidi kwa wachezaji wanaofanya ukiukwaji mkubwa wa nidhamu, hata kama tayari wamefungiwa kwa mujibu wa kadi walizopata.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, jukumu la kufuatilia adhabu za wachezaji lipo mikononi mwa Shirikisho la Soka la taifa husika pamoja na klabu yenyewe. CAF hutoa orodha ya wachezaji waliopigwa marufuku kabla ya kila mechi, lakini klabu ikimchezesha mchezaji ambaye amezuiwa, matokeo yanaweza kubatilishwa.

Wakati Simba hali ikiwa hivyo, wapinzani wao Stellenbosch kuna nyota watatu wa kikosi cha kwanza wenye kadi mojamoja za njano ambao wote wanacheza eneo la ulinzi. Wachezaji hao ni kipa Sage Stephens na mabeki Enyinnaya Godswill na Ismaël Olivier Touré.

Timu zingine zilizoingia nusu fainali ya michuano hiyo, RS Berkane nayo ina wachezaji wawili wenye kadi mojamoja za njano ambao ni beki Haytam Manaout na kiungo Ayoub Khairi, huku CS Constantine ikiwa na nyota watatu wenye kadi mojamoja za njano ambao wote ni mabeki Laïd Chahine Bellaouel, Achraf Boudrama na Miloud Rebiaï.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *