Mastaa Pamba Jiji wamliza Minziro

KATIKA mahojiano maalumu na Mwanaspoti, kocha mkuu wa Pamba Jiji, Fredy Felix ‘Minziro’ kafichua jambo ambalo liliiua timu yake dhidi ya Yanga jana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, lakini akisema pamoja na kuvutwa shati kuna hesabu zao bado ziko sawa na wanapambana.

Minziro ameliambia gazeti hili kwamba, kukosa umakini katika safu ya ulinzi na kushindwa kutumia vyema nafasi zilizotengenezwa ndiyo sababu ya kikosi chake kupoteza kwa mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Yanga, jambo ambalo mazoezini wanenda ‘kufa’ nalo kuhakikisha kwamba halijirudii katika mechi zijazo.

Pamba Jiji ilikutana na kichapo hicho kutoka kwa Yanga baada ya kucheza michezo miwili mfululizo ya ligi katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na kushinda yote dhidi ya Azam FC (1-0) na Coastal Union (2-0).

Katika mchezo juzi, dakika 20 za kipindi cha kwanza, Pamba Jiji iliikamata Yanga na kutengeneza nafasi nne ambazo mshambuliaji wake raia wa Kenya, Mathew Tegis na kiungo Zabona Mayombya walikosa umakini katika uamuzi wa mwisho na mashuti yao kuishia mikononi kwa kipa wa Yanga, Djigui Diarra.

Miongoni mwa nafasi hizo ni ile ya dakika ya nne na 17 ambazo Mayombya aliwachambua mabeki wa Yanga, lakini akaishia kupiga michomo dhaifu. Pia kiungo, Yonta Camara katika dakika ya sita alipata nafasi kama hiyo akapiga nje ya lango, dakika ya 34 Tegis alipata nafasi ya dhahabu baada ya beki Ibrahim Bacca kuanguka na kupoteza mpira ambao aliunasa na kumchekecha Bakari Mwamnyeto, lakini akapiga shuti ambalo liliokolewa na Diarra.

“Naweza kusema kile tulichokipanga mazoezini wachezaji wangu hawakukitendea haki kwa sababu kama wangekitendea haki pengine mechi ingekuwa nzuri. Mechi tulikuwa tumeichukua mapema kipindi cha kwanza kama nafasi ambazo tulizipata tungezitumia vizuri hii ingekuwa bora katika mechi za Ligi Kuu ambazo zingekuwa bora sana,” amesema Minziro.

“Nafasi tumezipata hatukuzitumia vizuri. Kwa hiyo nadhani iliishakwisha wenzetu wamepata nafasi wamezitumia vizuri. Unapopata nafasi tatu au nne kwenye mechi kama hii halafu huzitumii vizuri kinachofuata lazima utaadhibiwa na ndicho kilichotokea.”

Minziro amesema kucheza na timu za daraja kama la Yanga unahitajika umakini mkubwa na kutofanya makosa ya lazima, huku akiamini mchezo uliwapa funzo na sasa nguvu wanahamishia mchezo dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba.

“Kila kitu kiko wazi ukikutana na wachezaji ambao ni daraja la juu lazima uwe vizuri kiakili, yaani unajipanga kutumia vizuri nafasi unazozipata unazitumia vizuri, halafu unajitahidi kuhakikisha haufanyi makosa yasiyokuwa ya lazima. Sisi hatukutumia nafasi zetu halafu tumefanya makosa ambayo yametugharimu,” amesema Minziro.

Baada ya kucheza mechi 22 za Ligi Kuu, Pamba Jiji inakamata nafasi ya 12 ikiwa na alama 22, ikishinda tano, sare saba na kupoteza 10, huku ikifunga mabao 13 na kuruhusu 23.

Matokeo ya Pamba chini ya Minziro msimu huu ni Kagera Sugar sare ya 1-1, ikaifungwa na Tabora United 1-0, ikashindwa na Namungo 1-0, ikaifunga Fountain Gate 1-3, ikapoteza kwa Simba 1-0, Ikaishinda Ken Gold 0-1, JKT Tanzania 0-0, KMC (1-0), ikafungwa na Tanzania Prisons 1-0, ikaishinda Dodoma Jiji 0-1, ikafunga Azama 1-0, ikaifumua Coastal Union 0-2, ikafungwa na Mashujaa FC 2-0, Singida Black Stars 2-2 na kufumuliwa na Yanga 3-0.

NANE ZILIZOBAKI PAMBA JIJI

Machi 7, 2025 v Kagera Sugar (Kaitaba, Bukoba)

Aprili 2, 2025 v Namungo  (CCM Kirumba)

Aprili 5, 2025 v Tabora Utd (CCM Kirumba)

Aprili 8, 2025 v Fountain Gate (CCM Kirumba)

Mei 8, 2025 v Simba (KMC Complex)

Mei 13, 2025 v Ken Gold (Sokoine, Mbeya)

Mei 21, 2025 v JKT Tanzania (CCM Kirumba)

Mei 25, 2025 v KMC (CCM Kirumba)