Manchester, England. Taarifa za ndani zinadai, Manchester United italazimika kuuza wachezaji nyota ili kupata fedha za kufanya maboresho makubwa ya kikosi chake katika dirisha lijalo.
Man United inahitaji kuboresha kikosi chake baada ya kuendelea kuwa na msimu mbaya siku hadi siku na kocha Ruben Amorim amewaambia mabosi wa timu hiyo kwamba anahitaji bajeti kubwa ya usajili kwenye dirisha lijalo.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 40 amekuwa akiweka wazi kwamba baadhi ya nyota hawaendani na matakwa ya mfumo wake wa 3-4-3 kiasi cha wengine kuwaanzishia benchi ikiwemo Alejandro Garnacho.

Amorim ambaye alipata mafanikio kupitia mfumo huo akiwa na Sporting Lisbon, ripoti yake anayotarajia kuiwasilisha kabla ya msimu kuanza inaonyesha wachezaji wengi hawapo katika mipango yake hususani eneo la ushambuliaji.
Minong’ono juu ya hili iliongezeka zaidi baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 2-0 katika mchezo ambao Amorim alimwanzisha kiungo Kobbie Mainoo kama mshambuliaji wa kati, huku Rasmus Hojlund na Joshua Zirkzee, ambao walisajiliwa kwa gharama kubwa wakiwa benchi.
Ripoti za mwezi uliopita zilidai kuwa karibu kikosi chote cha Man United kinaweza kuuzwa mwisho wa msimu na hata mwezi uliopita Alejandro Garnacho naye alikuwa na nafasi kubwa ya kuuzwa kwenda Napoli kabla ya dili lake kukwama kutokana na kiasi kikubwa cha pesa kilichotajwa na Man United.
Kuuzwa kwa wachezaji mbali ya kwamba hawapo katika mipango ya Amorim, pia inachangiwa na sheria za matumizi ya pesa zilizowekwa na mamlaka zinazosimamia Ligi Kuu England.
Garnacho anatarajiwa kuwa miongoni mwa wachezaji watakaolengwa na timu kubwa barani Ulaya, huku ripoti zikidai kuwa hata Mainoo yupo kwenye orodha ya wanaoweza kuuzwa.

Kwa mujibu wa The Guardian, Mainoo na Garnacho ambao walihusishwa kuuzwa katika dirisha la Januari watakuwa tena sokoni mwisho wa msimu.
Uuzaji wa wachezaji waliotoka kwenye akademi ya Man United kama Mainoo, Garnacho, na Marcus Rashford utahesabiwa kama faida ya asilimia 100 jambo ambalo litaiwezesha Man United kutumia kiasi kikubwa kwenye kusajili mastaa wengine ambao kocha anawahitaji.
Amorim tayari ameshaanza kupata wachezaji ambao anaona wanaendana na mifumo yake ambapo katika dirisha lililopita mashetani hao wekundu walilipa pauni 25 milioni kwa aijili ya kumsajili beki wa kushoto wa Lecce, Patrick Dorgu pamoja na kinda wa Arsenal Ayden Heaven.