TIMU ya Soud Black imetwaa ubingwa wa Ramadhan Star League 2025 baada ya kuifunga Miyasi kwa pointi 64-41 katika fainali iliyofanyika kwenye Uwanja wa Donbosco, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Mashindano hayo ya mastaa yalishirikisha wachezaji nyota kutoka timu zinazoshiriki Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) waliounda timu nane na kuzipa majina ya wachezaji. Kundi A ilikuwa na Miyasi, Nahreel, Mwalimu, Evance huku lile la B lilikuwa na Soud Black, Mkosa, Mngeja na Labani.
Kutinga fainali kwa timu hizo kulitokana na Miyasi kuifunga Mkosa kwa pointi 71-69 katika nusu fainali, huku Soud Black ikiifunga Evance kwa pointi 69-50.
Kwa kubeba ubingwa wa mashindano hayo, Soud Black ilizawadiwa Sh3 milioni na Miyasi ikiondoka na milioni 1.5, huku mchezaji bora akichaguliwa kuwa Omary Sadick wa Soud Black.
Sadiki anayecheza kama namba moja yaani point guard ubora wake ulitokana na uwezo wa kutoa asisti kwa wachezaji wenzake na kufunga, ambapo nyota huyo anayechezea JKT kwenye BDL katika fainali hiyo alitoa asisti 10 na pasi mbovu mara mbili.
Na katika mchezo huo pia alifunga pointi 22, huku kati ya hizo akifunga ‘three pointi’ tisa akifuatiwa na Fotius Ngaiza anayeicheza Vijana ‘City Bulls’ aliyefunga pointi 15.
Kwa upande wa Miyasi alikuwa Mkongomani Marcus Tshi aliyefunga pointi 13 akifuatiwa na Yekonia aliyefunga 10.
Fainali hiyo iliyoshuhudiwa na watazamaji wengi ilichagizwa na uwepo wa mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko ambaye ni mmoja wa wadau na mastaa wa kikapu nchini.

Jesca Vs Tuku
Katika mashindano hayo Timu Jesca iliifunga Tuku kwa pointi 45-40 upande wa mastaa wa kike wa timu zinazoshiriki Ligi ya Kikapu ya Wanawake Mkoa wa Dar es Salaam (WBDL).
Tuku ilibeba ubingwa huo katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Donbosco, Oysterbay na hivyo kuzawadiwa Sh1.5 milioni.
Katika mchezo Tuku iliianza robo ya kwanza kwa kuidhibiti Jesca jambo lililowafanya wapinzani wao hao wapoteane, kwani inamalizika Tuku ilikuwa inaongoza kwa pointi 13-8, ilhali robo ya pili Jesca iliongoza pia kwa pointi 14-10.
Robo ya tatu, mchezo ulizidi kuvutia na Jesca iliongoza tena kwa pointi 14-13 huku ile ya nne ikipata pointi 9-4.
Katika mchezo huo, Noela Uwandameno alifunga pointi 13, akifuatiwa na Jesca Ngisaisa aliyefunga pointi tisa ilhaliupande wa Tuku alikuwa Tumwagile Joshua aliyefunga pointi 14 akifuatiwa na Jesca Mbowe aliyetupia nane.

Lengo vijana wacheze
Akizungumzia mashindano hayo, staa wa Bongofleva, Emmanuel Mkono alisema alichagua timu ya vijana wenye umri wa miaka 18 aliyoipa jina la Nahreel ili wacheze.
“Unajua wachezaji wadogo wakipata nafasi ya kucheza mashindano kama haya uzoefu wao unaongezeka,” alisema Mkono ajulikanaye kisanii kama Nahreel na kwamba hawezi kuwalaumu vijana hao kwa kiwango walichocheza katika mashindano hayo.
“Tulikosa kufunga pointi mara kwa mara tunapofika kwenye goli katika michezo yote tuliyocheza na uzoefu pia naona ulichangia kwa timu yangu kutolewa mapema,” alisema Mkono
Timu Nahreel ilipoteza michezo mitatu kwa kufungwa na Miyasi pointi 40-28, Evance 62-40 na Mwalimu 60-40.
Wakati huohuo, timu mpya ya wanawake ya The Reeelbasketball imeanzishwa kwa ajili ya kushiriki Ligi ya Kikapu ya Wanawake Mkoa wa Dar es Salaam (WBDL).
Mwanzilishi wa timu hiyo Emmanuel Mkono, alisema: “Kuomba kushiriki katika Ligi ya Kikapu Wanawake tumeomba kwa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD),” alisema Mkono.
Timu zinazotarajia kushiriki ligi hiyo upande wa wanawake ni Donbosco Lioness, Vijana Queens, JKT Stars, Jeshi Stars, Polisi Stars, Tausi Royals, UDSM Queens, DB Troncatti, Pazi Quees na Twalipo Queens.

Kikapu Wheelchair yachangiwa
Katika kile kilichoonekana ni kuguswa kwa wadau wa mchezo wa kikapu kwa timu ya watu wenye ulemavu, mashabiki wameichangia fedha katika mashindano hayo.
Wadau hao wameichangia zaidi ya Sh5 milioni ikiwa ni fedha taslimu na ahadi pamoja na vifaa vya michezo.
Bahati Mgunda, kocha wa kikapu, aliahidi kutoa mipira mitano na jozi sita za viatu kwa wachezaji – vitu ambavyo atakabidhi baada ya kukutana na uongozi timu hiyo.
Kabla ya kuchangiwa ulipigwa mchezo wa kikapu kwa wachezaji wenye ulemavu ambapo Malilo iliishinda Ashura kwa pointi 23-18.