Mastaa KenGold bado hawaamini

MATOKEO mabaya iliyonayo KenGold inayosubiri kwa sasa miujiza ili kuepuka kushuka daraja kutoka Ligi Kuu kurudi Ligi ya Championship, imewafanya hadi wachezaji wa timu hiyo kushindwa kuamini kilichowakuta, japo wameapa kupambana kupitia mechi nne zilizosalia ili kuona inakuwaje.

KenGold iliyopanda daraja msimu huu sambamba na Pamba Jiji, ndio inaburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 16 baada ya mechi 26 na imesaliwa na mechi nne ambazo kama itashinda zote itaifanya ifikishe 28 ambazo zimeshapitwa na Fountauin Gate iliyopo nafasi ya tisa kwa sasa.

Katika dirisha dogo lililopopita, KenGold ilifanya usajili wa kishindo wa kuongeza wachezaji wenye majina makubwa na uzoefu wa Ligi Kuu kama Obrey Chirwa, Kelvin Yondani, Zawadi Mauya, Bernard Morrison na wengine, lakini bado mambo hayajanyooka.

Kuyumba kwa KenGold kumeshtua hadi wachezaji wa timu hiyo akiwamo kipa Castory Mhagama.

“Kilichobakia kwetu kama wachezaji tunatiana nguvu kutokata tamaa. Tunapitia maumivu makubwa ya kukaa kwa muda mrefu mkiani,” alisema.

Timu hiyo katika mechi 26 imeshinda mara tatu tu, ikitoka sare saba na ikipoteza 16.

Alisema pointi 16 walizovuna zimekwamisha malengo yao na sasa wanasubiri chochote kitakachowakuta wakati Ligi ikifikia tamati Mei 25.

KenGold imebakiza mechi nne dhidi ya Coastal Union, Pamba Jiji, Simba na Namungo ikiwa na maana inasaka pointi 12 ambazo bado haziiweki timu hiyo salama kwa ajili ya kusalia kwa msimu ujao, hata kama wapinzani wanaochuana nao mkiani, Tanzania Prisons na Kagera Sugar wakacheza mechi zao.

“Tutapambana kushinda mechi zilizosalia bila kujiwekea malengo fulani, maana nafasi tuliyopo hatuna namna nyingine ya kusema chochote,” alisema  Mhagama na kuongeza;

“Hali tuliyonayo uisikie kwa mwingine, inafikia hatua unatamani angalau tupande japo nafasi moja juu ila imekuwa ni ngumu, hivyo ninachoweza kusema kwa sasa ni kushinda mechi tutasubiri nini kinafuata baada ya hapo.”

Timu hiyo iliyodumu mkiani kwa msimu mzima tangu ilipopanda Ligi Kuu baada ya kutwaa ubingwa wa Championship msimu uliopita inaongoza pia kwa kufungwa mabao mengi (48) ikiipiku Fountain Gate iliyokuwa inaongoza awali ambayo yenyewe imefungwa 47.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *