Dar es Salaam. Wiki inayoanza kesho dunia inakwenda kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake tukio ambalo hufanyika Machi 8 kila mwaka na kuhusisha makundi mbalimbali katika jamii kwa lengo la kuchochea usawa wa kijinsia.
Kwa kutambua uzito wa siku hiyo na umuhimu wake, tunakuletea orodha ya baadhi ya wanawake kutoka kiwanda cha burudani Bongo ambao wana mchango mkubwa katika tasnia hiyo na waweka rekodi za kipekee katika kazi zao kama ifuatavyo:
ROSE MUHANDO
Mwimbaji maarufu wa muziki wa injili tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000 na alikuwa msanii wa kwanza wa kike Tanzania kupata nafasi ya kusainiwa na lebo kubwa duniani, Sony Music Africa, dili ambalo alisaini Februari 2012.

Dili hilo lilimpa nafasi Rose kurekodi nyimbo mpya kwenye studio za Sony Music Africa zilizopo Afrika Kusini na wimbo wa kwanza kuutoa chini ya mkataba huo ni Wololo (2013) ambao uliidhinishwa na mtandao wa video za muziki wa Marekani, Vevo.
NANCY SUMARI
Hadi sasa Nancy ndiye mrembo mwenye historia yenye msisimko zaidi tangu kuanzishwa kwa Miss Tanzania baada ya kufanikiwa kutwaa taji la Miss World Africa (Continental Queen of Africa 2005) na ndiye Mtanzania pekee aliyefanya hivyo.

Nancy ambaye 2017 alitajwa katika orodha ya vijana 100 wenye nguvu ya ushawishi Afrika, amekuwa akitoa mafunzo ya matumizi ya vifaa vya kidijitali kwa watoto kupitia taasisi yake ya Jenga Hub na pia ameandika vitabu vinavyowahusu kama Haki, Nyota Yako na kadhalika.
LADY JAYDEE
Akiwa amerekodi nyimbo zaidi ya 200, kufanya kolabo zaidi ya 100 na kushinda na kutunukiwa tuzo zaidi ya 35 ndani ya miaka 15 mfululizo, Lady Jaydee anashikilia rekodi kama msanii wa kike wa Bongofleva aliyetoa albamu nyingi zaidi (nane).

Albamu yake ya kwanza Machozi (2001) yote ilirekodiwa MJ Records kwa Master J kisha zilifuata nyingine kama Binti (2003), Moto (2005), Shukrani (2007), The Best of Lady Jaydee (2012), Nothing But The Truth (2013), Woman (2017) na 20 (2021).
RITA PAULSEN
Huyu ni mkurugenzi wa Benchmark 360, kampuni inayosimamia shindano la kusaka vipaji vya uimbaji la Bongo Star Search (BSS), ambalo ndilo kongwe zaidi nchini kwa upande huo likifanyika kwa misimu 14 na kuibua wakali kibao.

Miongoni mwa wasanii walioibuliwa kwenye shindano hilo ni pamoja na Walter Chilambo, Peter Msechu, Haji Ramadhani, Kala Jeremiah, Frida Amani, Jumanne Iddi, Angel Kato, Kayumba na Phina ambaye ni mshindi wa tuzo nne za muziki Tanzania (TMA).
SEVEN MOSHA
Akiwa na uzoefu wa miaka zaidi ya 20 katika tasnia ya burudani, Seven Mosha ndiye mtu wa kwanza kuteuliwa kusimamia masoko na maendeleo ya wasanii Afrika Mashariki chini ya Sony Music Entertainment, nafasi aliyoanza kuitumikia tangu Desemba 2020.

Baada ya uteuzi huo, kwa hapa Bongo Sony Music iliwasaini Abigail Chams, Aslay na Young Luny, huku hapo awali Seven akifanya kwa ukaribu na wasanii kama TID, Lady Jaydee, Alikiba, Barakah The Prince na Ommy Dimpoz ambaye bado yupo naye Sony.
JACQUELINE WOLPER
Umaarufu wake ulikuja kutokana na kucheza filamu baada ya kupaji chake kuibuliwa na Ray Kigosi, ila Wolper ana upande mwingine nao ni kutokea katika video za muziki akiwa ndiye mrembo pekee Bongo aliyeonekana katika video nyingi zaidi.

Wolper ambaye sasa ni mama wa watoto wawili baadhi ya video ambazo kaonekana ni Sio Demu (Tundaman), Still (Quick Rocka), Pesa (Mr. Blue), Goma la Manzese (Tip Top Connection), Niambie (Harmonize), Ben Pol (Sio Mbaya) na Utanipenda (Diamond Platnumz).
HAMISA MOBETTO
Amefanya mitindo, muziki na filamu vyote hivyo vimemfanya kuwa ndiye mwanamke pekee Bongo mwenye wafuasi wengi zaidi Instagram akiwa nao milioni 12, huku akishika nafasi ya pili Afrika Mashariki nyuma ya Zari The Bosslady kutoka Uganda.

Kwa Bongo baada ya Hamisa anafuata Wema Sepetu, Jacqueline Wolper, Nandy, Aunty Ezekiel, Kajala Masanja, Gigy Money, Linah, Zuchu, Lady Jaydee, Monalisa, Amber Lulu na Queen Darleen, staa wa WCB Wasafi mwenye wafuasi milioni 4.3 Instagram.
Baada ya MJ Records kufanya kazi na wanaume kwa miaka mingi, waliamua kumsaini Shaa akiwa ndiye msanii wa kwanza wa kike kusainiwa na lebo hiyo ambayo alifanya nayo kazi kwa takribani miaka 10 na kuachia albamu yake ya kwanza.

MJ Records ambayo kwa mara ya kwanza ililisaini kundi la Wagosi wa Kaya linaloundwa na Dk John na Mkoloni, walimchukua Shaa baada ya kufanya vizuri katika shindano la Coca-Cola Popstar 2004 na kuunda kundi la Wakilisha akiwa na wenzake wawili.
WEMA SEPETU
Akinyakua taji la Miss Tanzania 2006, Wema ndiye mrembo maarufu zaidi katika historia ya shindano hilo. uUnaweza kupima umaarufu wake kwa kutazama idadi ya wafuasi alionao Instagram ambao ni milioni 11.7 na hadi sasa hakuna Miss Tanzania aliyefikia hata nusu yake.

Umaarufu wake uliongezeka baada ya kujitosa katika uigizaji – filamu yake ya kwanza kucheza ni A Point of No Return (2007) akiwa na hayati Steven Kanumba kisha zikafuata nyingine kama Family Tears (2008), Red Valentine (2009) na White Maria (2010).
Akiwa na miaka minne ndani ya Bongofleva tangu atambulishwe na WCB Wasafi, tayari Zuchu anashikilia rekodi kama msanii wa kike mwenye wafuasi wengi zaidi YouTube na aliyetazamwa zaidi katika mtandao huo Afrika Mashariki.

Ni wiki chache zimepita tangu Zuchu aweke rekodi ya kutazamwa YouTube mara milioni 800. Kwa ujumla Afrika Mashariki ametanguliwa na Diamond Platnumz ambaye ni wa pili Afrika nyuma ya Burna Boy wa Nigeria, kisha Rayvanny na Harmonize.