Mastaa hawa wape mpira tu!

WAKATI Yanga na Simba zikiendelea kupigana vikumbo nafasi mbili za juu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, kuna siri imejificha kwa nyota wa timu hizo, Stephane Aziz KI na Leonel Ateba.

Siyo Yanga na Simba tu, lakini kila timu katika ligi hiyo inapambana kuweka mambo sawa, lakini mastaa wa vikosi 16 vinavyoshiriki hawalali usingizi mzuri kwa sasa ikiwa ni katika duru la pili la lalasalama la mashindano hayo, kwani kila timu inatafuta kujiweka pazuri kwenye msimamo.

Siri hiyo ipo katika mikwaju yao ya penalti ambapo timu hizo kila moja imepiga saba kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, huku Aziz Ki akiongoza kwa kupiga nyingi akifuatiwa na Ateba.

Juzi Ijumaa wakati Aziz Ki akifunga hat trick dhidi ya KMC wakati Yanga ikishinda 6-0, kiungo huyo kati ya mabao yake hayo matatu aliyofunga, mawili yalitokana na mikwaju ya penalti ambapo sasa amefikisha sita, kati ya hizo amefunga nne na kukosa mbili, akifuatiwa na Ateba aliyepiga nne na kufunga zote.
Katika penalti za mastaa hao, Aziz KI amepiga nne za upande wa kulia wa kipa ambapo kati ya hizo amekosa moja iliyotokea katika kichapo cha timu hiyo cha mabao 3-1, dhidi ya Tabora United, Novemba 7, 2024, huku mbili za kushoto akikosa pia moja tu.

Penalti hiyo moja ya upande wa kushoto aliyokosa ni ile ya ushindi wa kikosi hicho wa mabao 4-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliopigwa Februari Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam.

Kwa Ateba mwenye mabao manane hadi sasa ya Ligi Kuu Bara ikiwa ndio msimu wake wa kwanza hapa nchini, manne kati ya hayo ameyafunga kwa penalti, huku jambo la kushangaza kati ya hizo zote amezipiga upande mmoja tu wa kulia wa kipa.

Simba ndio timu yenye rekodi nzuri ya kupata penalti zote saba ilizopata msimu huu ambapo mbali na Ateba aliyefunga nne, kiungo nyota wa kikosi hicho, Jean Charles Ahoua anafuatia akipiga tatu ambazo zote ameziweka kimiani.

Kwa upande wa Yanga, inazo penalti saba msimu huu sawa na wapinzani wao Simba ila kati ya hizo imekosa mbili ambazo zote ni za Stephane Aziz KI, huku moja pekee ikipigwa na Pacome Zouzoua, katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Wakati Simba na Yanga zikiongoza kwa penalti, Namungo FC inazo sita ikikosa mbili, akianza Moubarack Amza wakati timu hiyo ilipochapwa mabao 2-0 na Fountain Gate Agosti 29, 2024 na ile ya Djuma Shabani katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Coastal Union Septemba 17, 2024.

Tabora United inafuatia kuwa na penalti tano na kati ya hizo imekosa moja tu, iliyopigwa na mshambuliaji Heritier Makambo, wakati kikosi hicho kilipochapwa mabao 3-1 dhidi ya Fountain Gate, mechi iliyopigwa Septemba 20, 2024.

Timu nyingine ni Coastal Union yenye tano kabla ya jana kucheza na Pamba Jiji, kati ya hizo imekosa moja kupitia mshambuliaji Maabad Maulid wakati kikosi hicho kiliposhinda bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, mechi iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, Oktoba 29, 2024.

Singida Black Stars inazo nne na kati ya hizo imekosa mbili ambazo zote ni za mshambuliaji, Mkenya Elvis Rupia akianza na ile ya ushindi wa kikosi hicho wa mabao 2-1 dhidi ya KenGold, kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida, Desemba 24, 2024.

Nyingine aliyokosa nyota huyo ambaye ana mabao manane hadi sasa ni ile iliyoshuhudia kikosi hicho cha Singida kikichapwa mabao 2-0 dhidi ya KMC, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Februari 10, 2025.

Azam FC kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Mashujaa, ilikuwa na penalti tatu ikifunga zote sawa na Fountain Gate ila imekosa moja ya beki, Nicholas Gyan, wakati timu hiyo ilipochapwa mabao 2-1 dhidi ya Namungo, mechi ikipigwa Desemba 25, 2024.

KenGold inayoburuza mkia na pointi zake 10 baada ya kucheza michezo 19, ina penalti tatu pia msimu huu na kufunga zote, huku Mashujaa FC, Dodoma Jiji, Tanzania Prisons na Kagera Sugar ziwa na mbili kila mmoja wao na kutupia kambani zote. KMC FC na Pamba Jiji ndio timu mbili pekee kati ya 16, zinazoshiriki Ligi Kuu msimu huu ambazo hazina penalti hadi sasa. Hiyo ni kabla ya jana Pamba Jiji kucheza dhidi ya Coastal Union.

Kabla ya mechi mbili za jana, zimepigwa penalti 54 msimu huu katika Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hizo zimefungwa 44 na kukoswa 10, ikivuka idadi ya msimu uliopita wa 2023-2024, ambao jumla ya penalti 46, zilipigwa huku katika hizo zikifungwa 35, wakati zile zilizokoswa zilikuwa 11.

Rekodi ya penalti msimu huu inaweza kuivuka ile ya 2022-2023, ambapo jumla ya penalti 57 zilipigwa na kati ya hizo 40, ziliwekwa kimiani na 17 zilikoswa, huku kwa msimu wa 2021-2022 zilipatikana 50 na 32 zilifungwa wakati 18 zilikoswa.