Mastaa Bongo watoa neno Mfungo wa Ramadhan

Dar es Salaam. Mfungo  wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan umeanza leo Jumapili na waumini wa dini ya Kiislam duniani kote wanatimiza ibada hiyo ambayo ni moja ya Nguzo Tano za dini hiyo.

Ikiwa ni Nguzo ya Nne, waislamu hufunga kwa kujizuia kula na kunywa na kujikita katika kufanya ibada na mambo mema na kuepuka yale mabaya.

Katika kipindi hichi cha mwezi mmoja wa kufanya toba (Mfungo) wapo waumini ambao hubadili mtindo wa maisha na matendo na baadhi ya wasanii wa muziki, maigizo nchini wamezungumzia kipindi hiki cha mfungo na jinsi walivyoupokea.

MF 01

Gabo Zigamba

Msanii huyu wa filamu ambaye majina yake halisi ni Salim Ahmed anasema;

“Nashukuru mimi ni mmoja wa watu wanaofunga Mwezi wa Ramadhan. Nawashauri waislamu wote wasiache kufunga, kwani ni moja ya nguzo za uislamu na kwa wale wenzetu wenye imani nyingine basi waonyeshe nidhamu katika mizunguko yao ili kuepusha vishawishi kwa watu wanaofunga.”

Dulla Makabila

Mkali huyo wa muziki wa Singeli, Abdallah Ahmed ‘Dulla Makabila’ alisema;

“Mwezi wa Ramadhan nimeupokea vyema na salama na ninafunga maana ni moja ya nguzo ya Kiislamu, hivyo nawatakia kila la kheri Waislamu wote na wasio Waislamu katika kipindi hiki. Pia nawakumbusha tu kufunga na ibada ni muhimu sana.

“Pia naomba kwa Mungu nisipate changamoto niliyokumbana nayo mwaka jana katika kipindi hiki cha Mwezi wa Ramadhan kwenye kazi yangu ya muziki, maana nilipata shinikizo kutoka kwa waandaaji wa matamasha ya muziki wakati nilipokataa kufanya maonyesho wakati nikiwa kwenye mfungo,” alisema Dulla na kuongeza;

“Waandaaji wa matamasha wamekuwa wakinijia na ofa za fedha kwa ajili ya kujikimu kipindi hicho, ambacho ni kinyume na mafundisho ya dini yangu, yaani ilikuwa kila nikitaka kukataa shoo kwa ajili ya Mwezi wa Ramadhan, wenye shoo wanaongeza hela. Nikiendelea kukataa, asubuhi inafika naombwa hela za futari hadi nikasema Mungu anisamehe kipaji amenipa mwenyewe.”

MF 02

Sir Juma Nature

Mkongwe huyu wa muziki wa kizazi kipya ambaye majina yake halisi ni Juma Kassim Kiroboto a.k.a Kibla anasema;

“Ramadhan kareem kwa wote tuliofanikiwa kuuona mwezi mtukufu wa Ramadhan, In Shaa Allah, nimeupokea vizuri sana na nafunga kama kawaida yangu kila mwaka, ila nawashauri wasanii wenzangu na hata wasio wasanii, tujaribu kujiheshimu kimavazi na hata kimaongezi ili kulinda swaumu zetu.

Pia isiwe kwa mwezi huu tu bali hata miezi mingine tufanye hivyo na nipo jikoni kuachia ngoma yangu kuhusu mfungo wa Ramadhani kama nilivyofanya mwaka juzi na wimbo wa ‘Assalam Alaykum’ ikiwa ni mahususi kwa ajili ya Ramadhan.”

MF 03

Isha Mashauzi

Nyota huyu wa muziki wa taarabu anasema; “Nashukuru mwezi mtukufu umetufanya tufanye toba ya kweli na hata madhambi tuliyokuwanayo naamini baadhi yatakuwa yamefutwa kabisa.”

“Nashukuru Mungu kwa kunipa afya njema ya kufunga Ramadhan, nilikuwa namuomba Mungu, mwezi huu unikute salama wa afya ili nisiache kufunga, ili kama kuna baadhi ya makosa niliyowahi kuyafanya anisamehe.

“Kwa upande wa kufanya shoo kwa kipindi hiki, siwezi japo natafuta riziki, ila unajua hata riziki Mungu ndiye hupanga, hivyo kama hajapanga mimi kupata hata nikifanya shoo kipindi hiki sitapata kitu, hivyo nikuambie tu ukweli, kwa kipindi cha mfungo siwezi kufanya shoo hadi mfungo utakapoisha ndiyo nitaendelea kama kawaida na hii kwangu si mwaka huu tu bali huwa nafanya hivi kila mwaka.”

MF 04

Muumini Mwinjuma

Kiongozi wa Special Band ‘Tam Tam’, Prince Mwinjuma Muumin ‘Kocha wa Dunia’ kwa upande wake anasema;

“Mwezi huu nimeupokea vizuri kabisa na huwa naupenda sana kutokana na asilimia kubwa ya watu kubadilika kimavazi na hata kuzidisha ibada. Napenda huu mwezi ungekuwa kwa miezi yote 12, ingependeza kabisa yaani umetufanya tufanye toba ya kweli na hata madhambi tuliyokuwanayo naamini baadhi yatakuwa yamefutwa kabisa.

“Kwa ilivyokuwa mwezi huu, ndiyo bora wa miezi yote, hivyo basi mema yafanywayo ndani yake yanakuwa ni bora na yanalipwa ziada kuliko miezi mingine. Hivyo inatakiwa kwa muislam kujibidiisha katika kufanya mema na kuepuka mabaya hasa awapo ndani ya mwezi huu mtukufu. Baadhi ya mambo tutakiwayo tuyatekeleze.”

MF 05

Mzee Yussuf

Nyota wa muziki wa taarabu nchini, Mzee Yusuf anasema; “Nashukuru nimeupokea vyema mwezi wa Ramadhan na nafunga maana ni moja ya nguzo ya Kiislamu, hivyo nawatakia kila la kheri Waislamu wote na wasio Waislamu katika kipindi hiki.

“Nawakumbusha tu kufunga na ibada ni muhimu sana na hata unapomalizika watu waendelee na huu utarabu walionao sasa hivi, maana watu wengi mwezi ukiisha wanasahau kuswali na kumrejea muumba wao kama ilivyokuwa kwenye hii Ramadhan.”

MF 06

Msaga Sumu

Mtunzi na mwimbaji wa muziki wa singeli nchini, Seleman Jabir  ‘Msaga Sumu’ anasema; “Nimeupokea mwezi wa Ramadhan vizuri sana na nafunga kama kawaida yangu kila mwaka, ila nawashauri wasanii wenzangu na hata wasio wasanii tujaribu kujiheshimu kimavazi na hata kimaongezi ili kulinda swaumu zetu. Pia isiwe kwa mwezi huu tu bali hata miezi mingine tufanye hivyo tuzidishe kufanya ibada hali ya kuwa na imani na kutaraji thawabu anasamehewa yote yaliotangulia miongoni mwa makosa yake.”

MF 07
MF 07

Khadija Kopa

Malkia wa Mipasho na mmoja ya waimbaji nyota wa muziki wa taarabu nchini, anasema;

“Mie sina maneno mengi kwa huu mwezi mtukufu wa Ramadhan, zaidi ya kuwaasa tu wenzangu pamoja na watu wengine, Ramadhan isihamie mitandaoni, wanaofanya hivyo wanakosea, wajue tu kufunga ni imani na kusali ni imani, pia mwezi wa Ramadhani hauna kitu ambacho kama haujafanya hivyo haujafunga, mimi nimefunga kwa kuwa kinachofunga ni imani yangu na roho, tusimuigizie Mungu tuwe wa kweli, tusifanye kwa kumuogopa fulani.”

MF 09

Hamisa Mobetto

Mwanamitindo Hamisa Mobetto na mume wa nyota wa Yanga, Stephane Aziz KI, anasema;

“Ukweli kabisa bila ya kupepesa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan watu watumie fursa ya kusameheana pale walipokoseana.”

“Sioni haja ya watu au wasanii kuendelea kulumbana hasa katika mwezi huu mtukufu wa toba kwani haileti picha nzuri kwa jamii inayotuzunguka na kutufuatilia kuona kila siku tunakoseana. Nawaomba wasanii wenzangu kwa jumla pamoja na mashabiki zetu tusameheane kwa kuwa tunajenga nyumba moja, hivyo hatupaswi kuwekeana kinyongo.

“Mimi nilianza hivyo mapema kwa watu niliowakosea na walionikosea na ndiyo maana hata siku ya harusi yangu mliona watu ambao nilitofautiana nao walihudhuria, tujaribu kujishusha ili mambo yaende sawa na sio mwezi huu tu hata miezi mingine iwe hivyo.”