Mastaa Bongo wanavyoguswa tatizo la afya ya akili

Dar es Salaam.  Kwa ujumla kumekuwa na tafiti mbalimbali duniani juu ya afya ya akili ikielezwa kati ya watu 10, wanne miongoni mwao wanakabiliwa na changamoto hiyo.

Kutokana na hali hiyo, suala la afya ya akili limekuwa likijadiliwa katika muktadha mbalimbali, lakini halionekani kupungua na katika miaka ya karibuni likiongezewa uzito na mambo ya kiuchumi na wengi wanakumbana na kuathirika na hali hiyo.

Hata hivyo, kwa upande mwingine kinachowawia ugumu watu maarufu kama wasanii na wanasoka, ni jamii kushindwa kutofautisha kazi na maisha yao binafsi, jambo lililowasababishia baadhi yao kukumbwa na ugonjwa wa afya ya akili.

AK 01

Mwananchi imezungumza na baadhi yao na mtaalamu wa saikolojia ili kujua kipi kifanyike kuepukana na tatizo hilo au mtu akiziona dalili hizo afanye kitu gani.

Bohari ya Dawa (MSD), ikiwa ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Afya ambayo ilianzishwa 1993 kwa Sheria ya Bohari ya Dawa kama ilivyorekebishwa 2021, imefafanua kuhusiana na afya ya akili, ikieleza kwamba visababishi vyake ni mchanganyiko wa mambo mengi kama sababu za kurithi  yaani kama mtu yupo katika ukoo au familia, msongo wa mawazo, mazingira na utamaduni anaoishi na matatizo ya afya yanayoathiri ubongo.

MSD imetaja aina za ugonjwa huo kuwa ni wasiwasi, magonjwa ya hali kama vile kuwa na huzuni sana (mfadhaiko) au shauku sana (wazimu), matatizo ya haiba na ya kushindwa kudhibiti mawazo na misukumo.

AK 02

Wapo baadhi ya wasanii waliojitokeza kuelezea changamoto hiyo baada ya kuwakumba na baadaye kukaa sawa na mfano wa hivi karibuni ni nyota wa komedi, Gladness Kifaluka ‘Pili wa kikundi cha Kitimtim aliyeeleza katika mitandao ya kijamii kukumbwa na tatizo hilo na alivyopitia kipindi kigumu.

Pili anasema alikumbwa na hali hiyo iliyomfanya afikie mahala akawa haelewi kulikoni anaishi!

Mwingine ni msanii hip hop, Rosa Ree aliyewahi kuhijiwa na mojawapo ya vyombo vya habari nchini akakiri kukumbwa na changamoto hiyo na msaada wa watalamu wa akili na madaktari ndio waliomsaidia.

Baada ya mastaa hao kujitokeza Mwananchi imewatafuta wengine ili kuzungumza nao juu ya changamoto hiyo na jinsi zilivyowaanza na njia walizopitia kurejea katika hali yao ya kawaida.

Msanii mkongwe wa Bongo Fleva, Ferooz Mrisho, anasema tangu akiwa mdogo alikuwa anakumbwa na changamoto mbalimbali za kiakili lakini kinachomsaidia anasoma sana vitabu vinavyompa mwongozo wa kipi afanye ili asizame katika dimbwi jingine la mawazo.

AK 05

“Nasoma sana vitabu kama ‘Managing Stress’ ambavyo vinatoa maelekezo y nini ukifanye ili kuepukana na hali hiyo… vitabu vya mashairi. Siwezi kuvitaja vyote ni vingi sana. Nimepata ufahamu wa kuandaa kitabu cha maisha yangu ambayo yatawafunza wengine,” anasema Ferooz.

“Ukiwa staa watu wanapenda uishi maisha yao, lakini silikubali hilo, naishi uhalisia wangu… siwezi kuogopa kupanda bajaji, kuvaa nguo zilizopo ndani ya uwezo wangu”.

Msanii wa filamu, Julius Charles anasema akiwa na umri wa miaka 16 kwao Mwanza kutokana na urefu wake jamii ilikuwa haimuoni kama mtu wa kawaida na ilimfanya ajifungie ndani na kwamba aliyekuwa anampa moyo ni mama yake mzazi aliyemtaka  awe anatembea mtaani ili azoeleke.

AK 04

“Mama yangu mzazi na kupenda michezo kumenisaidia kujiona wa kawaida na sasa hadi nimepata nguvu ya kuingia katika mahusiano ambayo niliyaanza nikiwa na miaka 27, na sasa nina umri wa miaka 30,” anasema.

AK 03

Namna ya kuepuka 

Mwanasaikolojia Charles Nduku anataja namna ya kuepukana na changamoto hiyo endapo mhusika akiona dalili.

Nduku anasema mtu anayejiona katika hali hiyo anapaswa kuwahi hospitali na kukutana na watalamu wa saikolojia ili apate tiba kupitia ushauri.

“Mhusika anaweza akasaidiwa kwa kuzungumza naye na kushauriwa njia za kuepukana na hilo. Ndio maana wengine wanarudi katika nyumba za ibada, kusoma vitabu, kujichanganya na watu ili kukosa muda wa kuwaza ambako kunamsababishia ugonjwa wa afya ya akili,” anasema Nduku.