Mastaa Bongo waliotakata robo ya mwaka 2025

Dar es Salaam. Hatimaye robo ya kwanza ya mwaka 2025 imetimia huku mengi yakijiri katika tasnia ya burudani Bongo ambayo imesheheni mastaa wenye nguvu kubwa ya ushawishi inayotokana na umaarufu wa kazi zao.

Kwa kipindi hicho kuna mastaa waliotakata vilivyo kutokana na yale waliyofanikisha katika kazi zao na hata maisha yao binafsi kama ifuatavyo.

Diamond tuzo tatu za kimataifa

Staa wa Bongo Fleva kutokea WCB Wasafi, Diamond Platnumz tangu mwaka huu umeanza tayari ameshinda tuzo tatu za kimataifa alizowania akiwa msanii pekee nchini mwenye mafanikio hayo hadi sasa.

Diamond ameshinda tuzo za Trace 2025 zilizofanyika Zanzibar kama Msanii Bora wa Kimataifa Afrika, kisha akashinda Galaxy Music (Nigeria) kama Msanii Bora Afrika, na Irawna (Jamaica) kama Mtumbuizaji Bora wa Afrobeats.

Ndoa ya Hamisa na Aziz Ki

Baada ya tetesi za muda mrefu, hatimaye Februari 16 mwanamitindo Hamisa Mobetto alifunga ndoa na Stephane Aziz Ki ambaye ni mchezaji wa Yanga SC na Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Wawili hao ambao rasmi walithibitisha uhusiano wao hapo Agosti 2024 katika tuzo za TFF, shughuli yao nzima iliteka sana mijadala mtandaoni kuanzia tukio la utolewaji mahari, ndoa kufungwa na harusi yenyewe ambayo ilihudhuriwa na mastaa kibao.

Darassa na albamu ya pili

Rapa kutoka Classic Music Group (CMG), Darassa hapo Februari 7 aliachia albamu yake ya pili, Take Away The Pain (2025) ikiwa na nyimbo 15 huku akiwashirikisha wasanii kama Alikiba, Harmonize, Zuchu, Jay Melody na Mbosso.

Utakumbuka albamu yake ya kwanza, Darassa, Slave Becomes a King (2020) ilifanya vizuri na miongoni mwa nyimbo zake ‘Loyalty’ akiwashirikisha Marioo na Nandy, ulishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2021 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana.

Joti kung’aa tuzo za TCA

Katika tuzo za ucheshi, Tanzania Comedy Awards (TCA) 2025 zilizofanyika kwa mara ya kwanza, Joti aliyejizolea umaarufu kupitia kundi la Original Comedy, ndiye mchekeshaji pekee mkongwe aliyeng’aa zaidi akishinda tuzo mbili.

Hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa The Superdom Masaki hapo Februari 22 huku Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mgeni rasmi, Joti alishinda vipengele viwili ambavyo ni Mchekeshaji Bora wa Mwaka na Muigizaji Bora Mkongwe wa Mwaka.

Jux na Priscilla wafunga ndoa

Mwimbaji wa Bongo Fleva, Jux na Priscilla kutokea Nigeria waliweka wazi uhusiano wao mnamo Julai 2024 na kufika Februari 8 mwaka huu wakafunga ndoa iliyodhuriwa na mastaa wachache nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar es Salaam.

Utakumbuka Priscilla ambaye ni binti wa mkongwe wa Nollywood, Iyabo Ojo aliolewa na Jux miezi michache baada ya kuonekana katika video ya wimbo wa staa huyo, Ololufe Mi (2024) akimshirikisha Diamond ikiwa ni kazi ya tatu kufanya pamoja.

Aunty na mtoto mwingine

Staa huyu wa filamu mwanzoni mwa Machi yeye na mpenzi wake Kusah waliweka wazi kujaliwa kupata mtoto wao wa pili ila akiwa wa tatu kwa Aunty Ezekiel ambaye mtoto wake wa kwanza alizaa na dansa wa Diamond, Mose Iyobo.

Utakumbuka kuwa wawili hao wamekuwa wakishirikiana katika kazi zao za sanaa, mfano Aunty ametokea katika video ya Kusah, I Wish (2021) ambayo imetazamwa zaidi ya mara milioni 18 YouTube ukiwa ni wimbo wake wa kwanza kufanya hivyo.

Nandy, Jux washinda Trace

Katika tuzo za Trace 2025 zilizofanyika nchini kwa mara ya kwanza hapo Februari 26, Nandy kutokea The African Princess Label, alishinda kipengele cha Msanii Bora wa Kike Tanzania, huku Jux akishinda kama Msanii Bora wa Kiume.

Pia walipata nafasi ya kutumbuiza pamoja na mastaa wengine Bongo kama Diamond, Harmonize, Marioo na Zuchu huku Alikiba akiondoka bila kufanya hivyo na hali ya hewa ikitajwa kupelekea uamuzi huo mgumu.

Marioo kumjengea mama

Mwimbaji Marioo hapo Machi aliweka wazi kukamilika kwa nyumba ambayo amemjengea mama yake na kusema hiyo ni hatua kubwa kwake maana waliwahi kuishi chumba kimoja cha Sh15,000 huko Kiwalani, Dar es Salaam.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *