Mastaa Azam wafyekwa bonasi, wapewa saba za kujitathimini

KUTOLEWA katika Kombe la Shirikisho hatua ya 32 ikiwa ni mara ya kwanza kwa Azam FC, huku ikiwa na nafasi finyu ya kubeba taji la Ligi Kuu msimu huu, kumewafanya mabosi wa klabu hiyo kuitisha kikao cha dharura kilichotoa maazimio mawili na utekelezaji umeanza katika mechi iliyopita ya ligi dhidi ya TZ Prisons  Machi 6 na kushinda 4-0.

Azimio la kwanza ambalo uongozi wa Azam umeliamua ni kufuta bonasi zote za fedha ambayo ilikuwa inatoa kila timu inapoibuka na ushindi na wakati mwingine hata sare kutegemeana na uzito wa mechi.

Lakini baada ya kupoteza mechi ya Kombe la Shirikisho mbele ya Mbeya City kwa penalti 4-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1, wachezaji wa Azam hawatawekewa tena zawadi ya fedha katika mechi zilizosalia hadi msimu utakapoisha.

Kiwango cha chini ambacho wachezaji wa Azam wamekuwa wakipata kwa ushindi ni Sh10 milioni nacho huwa kwa mechi za kawaida lakini zipo mechi ambazo mabosi wa timu hiyo huweka hadi zaidi ya Sh100 milioni kama mbinu ya kuwapa hamasa mastaa wa kikosi chao lakini kwa sasa wameamua kutofanya hivyo.

Azimio la pili ni kupiga panga idadi kubwa ya wachezaji wa kikosi hicho hasa wale ambao wanaonekana kutokuwa na mchango ndani ya timu hiyo hivyo wamepewa mechi saba kupigania hatima zao, chanzo cha ndani kimeeleza.

Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Azam kimefichua kwamba wachezaji wa Azam kila mmoja ametakiwa atumie vizuri mechi saba ambazo zimebakia kwenye ligi kulinda nafasi yake kikosini.

“Mabosi hawakufurahishwa sana na yale matokeo dhidi ya Mbeya City hivyo wameamua kwamba kuanza mchezo dhidi ya Tanzania Prisons na mingine yote iliyobakia msimu huu, hakutokuwa na bonasi kwa timu hadi msimu utakapomalizika na kocha ameambiwa hizi mechi zilizobakia azitumie kuangalia mchango wa wachezaji kwenye timu.

“Wachezaji ambao watafanya vizuri watabakishwa kikosini na wale ambao viwango vyao havitaridhisha, wataonyeshwa mlango wa kutokea,” kilifichua chanzo hicho.

Kabla ya kupata ushindi wa mabao 4-0, Azam ilicheza mechi nne mfulizo za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho bila kupata ushindi.

Ilianza kutoka sare tasa dhidi ya Coastal Union kisha ikapata matokeo ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Simba na mchezo dhidi ya Namungo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 kisha ndipo ikatolewa Kombe la Shirikisho na Mbeya City ambayo sasa imepangwa kukutana na Mtibwa Sugar katika hatua ya 16 Bora.