
Nyota wanne waliowahi kutamba katika soka barani Afrika na duniani, leo watashiriki kuchezesha droo ya upangaji wa makundi ya fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 ambazo timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ni miongoni mwa timu shiriki.
Wakongwe hao ni Mustapha Hadji, Serge Aurier, Aliou Cisse na Joseph Yobo.
Mustapha Hadji anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa timu ya taifa ya Morocco ambayo aliitumikia hadi 2002 alipoamua kustaafu.
Katika mechi 63 alizoichezea Morocco, Hadji ameifungia mabao 12, akicheza fainali mbili za Kombe la Dunia.
Serge Aurier amecheza idadi ya mechi 93 za Ivory Coast akifunga mabao manne na alikuwepo katika vikosi vya nchi hiyo vilivyotwaa ubingwa wa Afcon mwaka 2015 na 2023.
Aurier amechaguliwa katika kikosi bora cha Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika mara nne mfululizo kuanzia 2015 hadi 2023.
Aliou Cisse anakumbukwa kwa kuiongoza Senegal kutwaa ubingwa wa Afcon mwaka 2021.
Joseph Yobo ni beki wa kati aliyecheza mechi 101 za timu ya taifa ya Nigeria kwa muda wa miaka 13 na ndiye alikuwa nahodha wakati timu hiyo inatwaa ubingwa mwaka 2013.