Mastaa 10 wanavyoisuta Manchester United

Machester. Manchester United imekuwa haifanyi vizuri katika mashindano mbalimbali inayoshiriki katika miaka ya hivi karibuni.

Matokeo hayo yasiyoridhisha uwanjani yamesababisha Manchester United kutimua makocha kadhaa huku pia ikiimarisha kikosi chake kwa kupunguza baadhi ya wachezaji na kuingiza wapya.

Pamoja na hilo, bado mambo yanaonekana kuwa magumu kwa timu hiyo ambayo miaka ya nyuma ilikuwa tishio ndani ya England na duniani kiujumla.

Baadhi ya nyakati, ilionekana kuna wachezaji wamekuwa chanzo cha kutofanya vizuri kwa timu hiyo na ikaonekana kuwafungulia mlango wa kutokea kunaweza kuwa suluhisho la timu hiyo kufanya vizuri lakini katika hali ya kushangaza, bado mambo hayaendi kama inavyotegemewa huku wachezaji hao wakionekana kutamba huko waliko kwa sasa na kudhihirisha kwamba kiwango kisichoridhisha chanzo chake sio wachezaji au makocha pekee.

Inavyoonekana kauli ya kukosekana kwa uhuru ndani ya Manchester United ina mashiko kutokana na maisha ambayo wachezaji 10 walio nje ya kikosi cha timu hiyo wanaishi kwa sasa.

Scott McTominay

Mambo yanaonekana kumuendea vizuri Scott McTominay ndani ya Napoli

Wapo kileleni mwa Serie A chini ya Antonio Conte na ameanza kila mechi ya ligi kando na mechi ya kwanza ya msimu huu huku akisifiwa sana kwa uchezaji wake.

Scott McTominay

Baada ya kuwa mchezaji wa kwanza raia wa Scotland kuwa ghali zaidi kuwahi kutokea baada ya uhamisho wa Pauni 26 milioni majira ya joto, amekuwa akionyesha Man United wanachokikosa kwake, akifunga mabao saba katika mashindano yote.

Mpenzi wake Cam Reading amehamia Italia na wawili hao wamekuwa wakiota jua na kufurahia vivutio vya utalii vya taifa hilo.

Anaonekana kufurahia maisha ya Italia na kudhihirisha hilo, mnamo Januari, McTominay alionyesha umahiri wake wa lugha alipomtakia Cam siku njema ya kuzaliwa… kwa Kiitaliano!

‘Buon compleanno Tutto il mio amore nel mondo,’ aliandika. Heri ya kuzaliwa Upendo wangu wote ulimwenguni.

Anthony Martial

Wengi walishangaa Martial alipokubali kujiunga na AEK Athens ya Ugiriki akiwa na umri wa miaka 28 baada ya kuondoka Manchester United mwezi Mei mwaka jana.

Sasa yuko kwenye kinyang’anyiro cha kuwania taji la Ligi ya Ugiriki, huku AEK wakiwa nyuma ya vinara Olympiacos kwa tofauti ya pointi mbili pekee.

Anthony Martial

Na baada ya kuanza polepole, Mfaransa huyo ameanza kujipata akifunga mabao tisa katika mechi 19 alizocheza.

Mwishoni mwa wiki, alifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Panserraikos.

Van de Beek

Ni miongoni mwa vipaji vilivyoanguka Old Trafford katika muongo mmoja uliopita.

Aliwasili kutoka Ajax akiwa na umri wa miaka 23 lakini aliondoka akiwa na umri mdogo wa miaka 27. Hakuweza kupata dakika za kucheza chini ya Ole Gunnar Solskjaer na hata uwepo wa Erik ten Hag, meneja wake wa zamani katika Ajax.

Sasa kiungo huyo ameanza kutamba takiwa Girona, kwenye Ligi Kuu ya Hispania ‘LaLiga’, huku akifurahia pia kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Aaron Wan-Bissaka

Ishara ya wazi zaidi ya Wan-Bissaka kuwa mchezaji aliyebadilika akiwa West Ham ilikuwa ni kufunga bao kwa mara ya kwanza baada ya siku 1,400.

Aaron Wan-Bissaka

Alipokuwa akikua, Wan-Bissaka alimtazama Thierry Henry kama staa anayevutiwa naye na kuvaa jezi yake namba 14.

Kwa sasa, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 anajisikia yuko nyumbani London, ikizingatiwa alizaliwa huko Croydon na akapitia timu ya Crystal Palace kabla ya kujiunga na Man United kwa pauni 50 milioni mwaka 2019.

Siku chache tu zilizopita, alichapisha ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram ukisomeka: ‘Daima Amani ni nzuri’.

Sofyan Amrabat

Amrabat aliwasili Manchester United kwa kishindo baada ya kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia akiwa na Morocco mwaka 2022 na fainali ya Ligi ya Europa akiwa na Fiorentina.

Sofyan Amrabat

Aliitumikia Manchester United kwa mkopo katika msimu wa 2023/2024 na kushindwa kuishawishi ibaki naye moja kwa moja.

Kwa sasa yupo kwa mkopo Fenerbahce, ambako ana nafasi kubwa ya kucheza chini ya kocha Jose Mourinho.

Alicheza dhidi ya Manchester United mapema msimu huu katika sare ya bao 1-1 kwenye Ligi ya Europa.

Jadon Sancho

Jadon Sancho ameonekana kurejesha makali yake akiwa na Chelsea.

Hivi karibuni mchambuzi wa soka, Danny Murphy, aliandika kuwa Sancho ‘anaonekana tena kama winga aliyeichezea Borussia Dortmund’.

Amepata nafasi ya uhakia ya kucheza upande wa kushoto wa timu hiyo inayonolewa na Enzo Maresca.

Ndani ya Manchester United, mchezaji huyo alionekana kama usajili ambao umesababisha upotevu wa fedha kutokana na kiwango kibov u ambacho alikuwa akikionyesha.

Kiasi cha Pauni 85.5 milioni ambacho Man United ilikitoa kwa Ajax ili kumsajili winga huyo ambaye kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 22, kilionekana kama fedha ambayo ilitupwa bila faida.

Anthony

Katika dirisha dogo msimu huu amepelekwa kwa mkopo Real Betis ambako amekuwa moto wa kuotea mbali akihusika na mabao mawili katika mechi mbili.

Raphael Varane

Ni miongoni mwa walinzi bora katika miaka ya hivi karibuni kabla ya kuamua kustaafu akiwa na umri wa miaka 31.

Baada ya kuitumikia Man United aliyojiunga nayo mwaka 2021 akitokea Real Madrid, katika dirisha kubwa la usajili mwaka jana alijiunga na Como ya Italia ambayo aliichezea mechi moja tu kabla ya kuamua kustaafu.

Kwa sasa amekuwa akitumiwa na klabu hiyo kufanya shughuli za kiutawala.

Tyrell Malacia

Baada ya kuteswa na majeraha ya mara kwa mara akiwa na Man United , mcheaji huyo amekuwa na msimu mzuri ndani ya PSV aliyojiunga nayo katika dirisha dogo la usajili, ambapo anatoa mchango kwa wababe hao wa Uholanzi kuwania taji la ligi na wapo pia katika mechi ya mtoano ya mtoano dhidi ya Juventus kwenye Ligi ya Mabingwa.

 Marcus Rashford

Baada ya kupita nyakati ngumu za kupishana na kocha Ruben Amorim huku kiwango chake kikibezwa na mashabiki wa Manchester United na wachambuzi wa soka England, mchezaji huyo aliamua kutimikia Aston Villa katika usajili wa dirisha dogo mwaka huu.

 Marcus Rashford

Inaonekana kama ndani ya Aston Villa atarudisha makali yake kwa vile kocha Unai Emery amemuahidi kumpa nafasi ya kutosha ya kucheza.

Kocha Emery alitamba kuwa Rashford amemuhakikishia kufanya vyema kupitia mazungumzo binafsi waliyofanya.

“Nina furaha naye sana. Mazungumzo niliyofanya naye yalikuwa mazungumzo ya kawaida sana kati ya mchezaji na kocha, tukizungumza kuhusu soka,” alisema Emery.