Masoud atuliza presha Chama la Wana

KOCHA wa Stand United ‘Chama la Wana’, Juma Masoud amewataka mastaa wa timu hiyo kuacha kuangalia kile ambacho wapinzani wao wakubwa Mtibwa Sugar na Mbeya City wanachokifanya, bali wawekeze nguvu katika kila mchezo wanaocheza sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Masoud alisema anachokitaka ni kuona wachezaji wanaendelea kupambana zaidi uwanjani kwa kila mchezo wanaocheza kwa sasa bila ya kuangalia wapinzani wao, kwa sababu kwa kufanya hivyo itawasaidia kuwaondolea presha.

“Presha ni kubwa sana hasa hii michezo iliyobakia na nafasi ambayo kila timu ipo na pointi ilizonazo, mimi sitaki kuona wakicheza kwa hali hiyo zaidi ya kuwataka kupambana hadi mwishoni mwa msimu kisha tutaangalia tutakapoangukia,” alisema.

Kikosi hicho kwa sasa kinashika nafasi ya tatu na pointi 52, baada ya kucheza michezo 24, kikishinda 16, sare minne na kupoteza minne, nyuma ya Mbeya City iliyopo ya pili sawa na pointi 52 na vinara wa ligi hiyo, Mtibwa Sugar yenye pointi 54.

Kocha huyo wa zamani wa FGA Talents (kwa sasa Fountain Gate), amejiunga na kikosi hicho akichukua nafasi ya Meja Mstaafu, Abdul Mingange aliyejiunga na Songea United, huku akiipambania kuirejesha Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2018-2019.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *