Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan, ameweka alama kubwa ya mafanikio katika maendeleo na ustawi wa sekta ya masoko ya mitaji, katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake mahiri.
Akielezea mafanikio makubwa yaliyopatikana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA. Nicodemus Mkama amesema, mafanikio hayo yametokana na mazingira wezeshi, shirikishi na endelevu ya kisera, kisheria na kiutendaji ya Serikali.
CPA. Mkama ameongeza kuwa sera za uchumi wa kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa zinazotekelezwa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia, zimekuwa chachu yenye matokeo chanya katika kukuza ushiriki wa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa na hivyo kuleta mafanikio makubwa zaidi katika masoko ya mitaji.
Sekta ya Masoko ya Mitaji imara, himilivu na yenye ufanisi mkubwa
Licha ya uwepo wa athari za migogoro ya kimataifa, masoko ya mitaji nchini yamekuwa salama, himilivu na yenye mafanikio makubwa, ambapo, thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 79.4 na kufikia Sh 52.3 trilioni katika kipindi kilichoishia Februari 2025, ikilinganishwa na shilingi trilioni 29.1 katika kipindi kilichoishia Februari 2021.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango akitoa pongezi kwa benki ya CRDB kukabidhiwa hati ya idhini ya hatifungani ya Miundombinu ya Samia kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu CMSA, Nicodemus Mkama.
Jumla ya mauzo ya hisa na hatifungani yameongezeka kwa asilimia 78.1 na kufikia Sh 25.8 trilioni katika kipindi kilichoishia Februari 2025, ikilinganishwa na Sh 14.5 trilioni katika kipindi kilichoishia Februari 2021 na thamani ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja imeongezeka kwa asilimia 454.6 na kufikia Sh 2.8 trilioni katika kipindi kilichoishia Februari 2025, ikilinganishwa na Sh 500.3 bilioni katika kipindi kilichoishia Februari 2021.
Tanzania yaweka rekodi ya bidhaa saba bunifu za kihistoria katika masoko ya mitaji
CMSA imetekeleza mikakati iliyowezesha utoaji wa bidhaa saba bunifu za kihistoria zinazovutia wawekezaji wa ndani na kimataifa. Utoaji wa bidhaa hizi ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa Njia Mbadala za Kugharamia Miradi ya Maendeleo (APF) uliozinduliwa na Mhe. Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wenye lengo la kuwezesha taasisi kutoka sekta ya umma na binafsi kupata rasilimali fedha za kugharamia miradi ya maendeleo.
Bidhaa hizo ni pamoja na; Hatifungani ya kwanza ya kijani yenye thamani kubwa iliyotolewa katika fedha mbalimbali, Kusini mwa Jangwa la Sahara, Hatifungani ya kwanza ya kijani ya taasisi ya umma kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji na utunzaji wa mazingira na Hatifungani ya kwanza yenye mguso wa jinsia Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Nyingine ni; Hatifungani ya kwanza yenye mguso na matokeo chanya kwa jamii, iliyotolewa katika fedha mbalimbali Afrika, Hatifungani ya kwanza inayokidhi misingi ya Shariah yaani Corporate Sukuk Bond na Hatifungani ya kwanza Iliyotolewa na shule ya sekondari na ambayo inayokidhi misingi ya Shariah
Hatifungani kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara vijijini na mijini
Masoko ya Mitaji Tanzania yamewezesha utoaji wa Hatifungani ya Miundombinu ya miaka mitano iitwayo Samia Infrastructure Bond kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara vijijini na mijini, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 323.09 kimepatikana, sawa na mafanikio ya asilimia 215.4.

Aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (wa pili kulia) akigonga kengele kuashiria uorodheshwaji wa hatifungani ya Tanga UWASA. Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Dk Natu Mwamba, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso na Afisa Mtendaji Mkuu CMSA, CPA. Nicodemus Mkama.
Lengo kuu la Hatifungani hii ni kuwawezesha wakandarasi wa ndani (local contractors) ambao wanafanya kazi na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) kuwa na uwezo wa kifedha ili kutekeleza kwa ufanisi na kwa wakati miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara. Hatifungani hii imeorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam, na imewezesha utekelezaji wa azma ya Mhe. Rais Samia ya kuimarisha miundombinu ya barabara nchini.
Mafanikio makubwa katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja
CPA. Mkama pia amesema, katika kipindi cha miaka minne, kumekuwa na maendeleo makubwa katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja, ambapo mifuko mipya inayotoa fursa kwa wawekezaji wa kada mbalimbali kuwekeza katika masoko ya mitaji imeanzishwa. Hatua hii imewezesha kuongezeka kwa thamani ya mifuko ya uwekezaji wa pamoja kwa asilimia 454.6 na kufikia Sh 2.8 trilioni, ikilinganishwa na Sh 500.3 bilioni mwaka 2021.
Mifuko mitano ya Uwekezaji wa Pamoja ya kampuni ya iTrust Finance Limited iitwayo iGrowth Fund, iIncome Fund, iCash Fund, iSave Fund na Imaan Fund
Mifuko miwili ya Uwekezaji wa Pamoja ya kampuni ya Sanlam Investments East Africa Limited iitwayo Sanlam Pesa Money Market Fund na Sanlam USD Fixed Income Fund.
Mifuko miwili ya Uwekezaji wa Pamoja ya kampuni ya Orbit Securities Limited iitwayo Inuka Fund na Orbit Index Fund.
Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa kampuni ya Watumishi Housing Investments uitwaoFaida Fund.
Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa kampuni ya Zan Securities Limited uitwao Timiza Fund.
Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa kampuni ya UTT AMIS PLC uitwao Juhudi Fund.
Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa kampuni ya Global Alpha Capital Limited uitwao Alpha Halal Fund unaowekeza katika bidhaa za masoko ya mitaji zinazokidhi misingi ya Shariah.
Matumizi ya teknolojia yaongeza wigo wa ushiriki wa wawekezaji aidha
CPA. Mkama amesema CMSA imewezesha kuanzishwa kwa mifumo bunifu ya uuzaji na ununuzi wa dhamana za masoko ya mitaji kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ikiwa ni pamoja na simu za mikononi na intaneti.
Jitihada hizi zimewezesha kuanzishwa kwa mifumo ya Sim Invest, Hisa Kiganjani, WekezaWHI na M-Wekeza ambayo inatumika kurahisisha upatikanaji wa huduma za masoko ya mitaji kwa wananchi wengi zaidi mijini na vijijini.
Ongezeko la wataalamu na taasisi zenye weledi na ujuzi wa viwango vya kimataifa
CPA. Mkama pia alibainisha kuwa, katika Kipindi cha miaka minne ya Mhe. Dk Samia, CMSA imetekeleza mikakati mbalimbali iliyowezesha kuongezeka kwa wataalamu wenye weledi na ujuzi unaotambulika kimataifa; kuongezeka kwa leseni zilizotolewa kwa kampuni zinazotoa huduma katika masoko ya mitaji na kuanzishwa kwa mpango wa mafunzo endelevu kwa watalaamu na watendaji katika masoko ya mitaji.
Wataalamu wa masoko ya mitaji wanaotambulika kimataifa wameongezeka kwa asilimia 82.8
Katika jitihada za kuongeza wataalamu wenye weledi na ujuzi wa k i m a t a i f a kwenye masoko ya mita j i , CMSA inashirikiana na Taasisi ya Uwekezaji na Dhamana ya nchini Uingereza (Chartered Institute for Securities and Investment, CISI) kutoa mafunzo yanayotambulika kimataifa kwa watendaji wa masoko ya mitaji hapa nchini.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.
Mafunzo haya yamewezesha idadi ya wataalamu wanaokidhi viwango vya kimataifa kuongezeka kwa asilimia 82.8 na kufikia 903 katika kipindi kilichoishia Februari 2025 kutoka 494 katika kipindi kilichoishia Februari 2021. Aidha, mafunzo haya yamewapatia wataalamu wa masoko ya mitaji fursa ya kupata leseni za kutoa huduma katika masoko ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Kampuni zenye leseni ya kutoa huduma katika masoko ya mitaji zaongezeka kwa asilimia 60.4
Utekelezaji wa mafunzo kwa watendaji wa masoko ya mitaji yanayotambulika kimataifa yamewezesha idadi ya watendaji wa masoko ya mitaji wenye leseni ya CMSA kuongezeka kwa asilimia 60.4 na kufikia 231 Februari 2025 kutoka 144 Februari 2021.
Kuongezeka kwa idadi ya watendaji wa masoko ya mitaji ni hatua muhimu katika kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wenye lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi.
Kuanzishwa kwa mpango wa mafunzo endelevu kwa wataalamu wa masoko ya mitaji
CMSA imeanzisha Mpango wa Mafunzo Endelevu kwa Wataalamu wa Masoko ya Mitaji (Continuous Professional Development Program, CPD) wenye lengo la kuhuisha uelewa na kujenga uwezo wa watalamu hawa kuhusu fursa mpya, mabadiliko, changamoto na masuala yanayoibuka siku hadi siku katika nyanja za masoko ya mitaji nchini na ulimwenguni kote.
Hatua hii ni muhimu katika kutekeleza mpango mkuu wa maendeleo ya sekta ya fedha wenye lengo la kujenga uwezo wa rasilimali watu katika sekta ya fedha.
Mafanikio katika kuongeza huduma jumuishi za kifedha
Sekta ya masoko ya mitaji imepiga hatua kubwa katika kuongeza huduma jumuishi za kifedha. Kuongezeka kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ikiwa ni pamoja na simu za mikononi, kumetoa wigo mpana kwa wawekezaji wa kada mbalimbali kushiriki katika masoko ya mitaji.
Aidha, kuanzishwa kwa ushirikiano baina ya watendaji wa masoko ya mitaji na benki za biashara, kampuni za simu na Shirika la Posta kumeongeza zaidi upatikanaji wa huduma za masoko ya mitaji, hususan jamii ambazo zilikuwa hazifikiwi kirahisi. Halikadhalika, CMSA imetekeleza programu mbalimbali za kutoa elimu kwa umma kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji. Programu zilizotekelezwa ni pamoja na:

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA. Nicodemus Mkama.
Kuendesha semina kuhusu masoko ya mitaji
CMSA imeendesha semina zenye lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu fursa na faida zinazopatikana kwenye masoko ya mitaji. Mada na semina hizo zimetolewa kwa makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vijana, vikundi vya wanawake, wajasiriamali, watunga sera, waheshimiwa wabunge, taasisi za umma na binafsi, makundi ya kijamii na watu wenye mahitaji maalumu.
Kushiriki katika maonyesho ya kitaifa na kimataifa
CMSA imeshiriki katika maonyesho ya kitaifa na kimataifa yenye lengo la kutoa elimu kuhusu fursa na faida zinazopatikana kwenye masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na Wiki ya Wawekezaji Duniani, Wiki ya Huduma za Fedha, Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba, Maonyesho ya Kimataifa ya Wakulima (NaneNane), Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Zanzibar na Maonyesho ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
Kuendesha mashindano kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu
CMSA imeendesha mashindano kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kuhusu masoko ya mitaji na uwekezaji. Mashindano hayo yameonyesha mafanikio makubwa kutokana na kuendeshwa kwa kutumia njia ya mitandao ya kielektroniki yaani simu za mikononi na intaneti.
Mashindano haya yamesaidia kuongeza elimu ya masoko ya mitaji kwa vijana wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ambapo idadi ya washiriki imeongezeka na kufikia wanafunzi 88,871 katika kipindi kilichoishia Februari 2025 kutoka wanafunzi 48,662 katika kipindi kilichoishia Februari 2021, ikiwa ni ongezeko la asilimia 82.6.
Mashindano haya yamekuwa na matokeo chanya kwa kuongeza idadi ya wawekezaji vijana 10,000 katika masoko ya mitaji; kuanzishwa kwa Jukwaa la Wawekezaji Vijana lenye wanachama zaidi ya 6,000 ambalo linawezesha wawekezaji vijana kupata elimu na uzoefu wa uwekezaji katika masoko ya mitaji. Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuwawezesha vijana kiuchumi.
Uwepo wa mazingira wezeshi ya kisheria na kiutendaji
CPA. Mkama pia amesema katika kuweka mazingira wezeshi ya kisheria, CMSA imetekeleza yafuatayo: imetoa Mwongozo ya kuendesha na kusimamia bidhaa za mitaji halaiki yaani Guidelines for Investment-based Crowdfunding, imetoa mwongozo wa utoaji wa hatifungani za sukuk kwa kampuni na taasisi za umma yaani na imefanya mapitio ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Sura 79 ya Sheria za Tanzania, ambapo maboresho yamefanyika kwenye Sheria kwa kuimarisha masharti ya kulinda maslahi ya wawekezaji wenye hisa chache katika kampuni za umma na zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa.
CPA. Mkama amehitimisha kwa kusema kuwa, Sekta ya Masoko ya Mitaji Tanzania ni imara na himilivu na kuwa CMSA itaendelea na jitihada zenye lengo la kuchagiza na kutoa mchango chanya katika kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu. CPA.
Mkama amemtakia Mhe. Rais Dk. Samia heri katika uongozi wake na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu afya njema, baraka na fanaka katika kutekeleza kazi ya kuleta maendeleo ya jamii na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.