
Kigoma. Yanga iko ugenini katika Uwanja wa Lake Tanganyika leo kuanzia saa 10:30 jioni katika mchezo wa ligi ambao hauonekani kuwa mwepesi kwa kila upande.
Sababu kuu ya ugumu wa mchezo huo ni nafasi ambayo kila moja ipo kwenye msimamo wa ligi na pointi ambazo imekusanya hadi sasa.
Kwa Yanga, ushindi wa leo utaihakikishia kuendelea kuongoza msimamo wa ligi ambapo itafikisha pointi 55 lakini pia itakuwa inajiweka katika mazingira yasiyo ya presha kuelekea mechi ya Kariakoo Dabi dhidi ya
Simba kwani baada ya leo itacheza mechi moja dhidi ya Pamba na baada ya hapo itakabiliana na mtani wake, Machi 8 mwaka huu.
Mashujaa ikipata ushindi leo, itafikisha pointi 26 ambazo zinaweza kuisogeza juu kwa nafasi moja hadi nafasi ya sita lakini kama itaangusha pointi leo, bado haitakuwa kwenye mazingira salama katika msimamo wa ligi.
Ni tofauti ya pointi tano tu ambayo inaitenganisha Mashujaa FC na timu iliyopo katika mstari wa kushuka daraja kwa sasa hivyo inalazimika kupata ushindi leo ili angalau iongeze pengo la pointi dhidi ya timu zilizo chini yake.
Katika mchezo wa leo, Yanga itapaswa kumchunga zaidi mshambuliaji wa Mashujaa FC, David Ulomi ambaye hadi sasa amepachika mabao manne katika Ligi Kuu.
Tishio zaidi kwa Mashujaa ni Clement Mzize ambaye anaongoza kwa kufunga mabao Ligi Kuu akiwa nayo 10 na Prince Dube ambaye hadi sasa amefumania nyavu mara tisa.
Katika Ligi Kuu Tanzania Bara, timu hizo zimekutana mara tatu ambapo Yanga imefanikiwa kuibuka na ushindi katika mechi hizo zote ambapo mechi ya kwanza ilipata ushindi wa mabao 2-1 ya pili ikashinda kwa bao 1-0 na ya tatu ikapata ushindi wa mabao 3-2.
Kocha wa Yanga, Hamdi Miloud amesema kuwa kilichowapeleka Kigoma ni ushindi na sio matokeo mengine.
“Kuhusu mchezo tunajua itakuwa ngumu na tunawajua wapinzani wetu na tunawaheshimu. Hatupo hapa kupumzika. Tupo hapa kushinda na kupata pointi tatu dhidi ya Mashujaa,” alisema Hamdi.
Kocha wa Mashujaa, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ alisema nafasi ambayo wapo kwenye msimamo wa ligi unawalazimisha wao kuhakikisha wanapata matokeo mazuri leo.
“Tunacheza na timu kubwa ambayo ina wachezaji wa kuamua matokeo. Lakini na sisi tumejipanga kwa namna ya kuweza kukabiliana nao.
Tunafahamu sisi bado hatupo salama kuna pointi ambazo tunahitaji kuongeza na wenzetu wanahitaji kuwa juu zaidi,” alisema Baresi.
Kabla ya mchezo wa Mashujaa na Yanga kutakuwa na mechi moja itakayochezwa mchana saa 8:00 mchana na saa 1:00 usiku kutakuwa na mchezo mwingine mmoja.
Mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu kwa siku ya leo utakuwa baina ya Singida Black Stars dhidi ya Pamba Jiji FC ambao utachezwa kwenye Uwanja wa CCM Liti, Singida.
Siku ya leo itamaliziwa na mechi ya saa moja usiku baina ya Namungo FC na Coastal Union katika Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi.