Mashujaa jana jioni ilikuwa uwanjani mjini Kigoma kuvaana na Pamba Jiji, huku timu hiyo ikiwa na rekodi ya kucheza dakika 720 bila ushindi, lakini kocha Mohamed Abdallah ‘Baresi’ ametamba kwamba hataki unyonge tena na amejipanga kuisapraizi Yanga wanaokutana nao Kigoma.
Mashujaa inayocheza Ligi Kuu kwa msimu wa pili sasa baada ya kupanda msimu uliopita, imecheza mechi nane bila kupata ushindi na jana ilikuwa inatesti zali kwa Pamba, lakini akili za Baresi zipo kwa mchezo wa Jumapili dhidi ya Yanga na kusema wamejipanga kutafuta matokeo mazuri nyumbani.

Baresi ameiambia Mwananchi kwamba, anajua ana kazi kubwa ya kufanya kuikabili Yanga ambayo ipo kileleni kwa ubora na wao wanapambana kutafuta matokeo mazuri baada ya kushidwa kufanya hivyo kwenye mechi nane zilizopita (kabla ya jana).
Mashujaa mara ya mwisho kushinda ilikuwa Novemba 23, mwaka jana ilipoifunga Namungo kwa bao 1-0 baada ya hapo wameambulia vipigo vinne na sare nne na baada ya kucheza jana sasa utakabiliana na Yanga Jumapili ya wikiendi hii kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika baada ya awali kulala 3-2 ugenini.
Akizungumzia mchezo huo ujao, Baresi amesema mpira ni mchezo wa makosa na mtu ukikosea kidogo unaadhibiwa wanaelewa ubora wa Yanga wanapambana kujiimarisha ili kuhakikisha wanabakiza pointi zote tatu nyumbani.
“Hautakuwa mchezo rahisi tutaingia kwa kuwaheshimu wapinzani wetu lakini huo mchezo kwetu ni muhimu sana tunazihitaji pointi tatu muhimu tukiwa kwenye uwanja wetu wa nyumbani,” amesema Baresi ambaye tangu timu hiyo ipande daraja haijawahi kushinda mbele ya vigogo, Simba, Yanga na Azam.
Timu hizo mzunguko wa kwanza Yanga ikiwa wenyeji ilishinda Mashujaa mabao 3-2 na rekodi za ugenini Yanga bado ni mbabe kwani mchezo wa mwisho wa msimu uliopita ilishinda bao 1-0 baada ya awali kuichapa mabao 2-1 Uwanja wa Azam Complex.
Kwa upande wa kocha wa Yanga, Miloud Hamdi aliyeiongoza timu hiyo katika michezo mitatu na kuvuna pointi saba amesema anaongoza kikosi chenye wachezaji wazoefu na wenye ubora ndio siri ya matokeo licha ya ratiba kuwanyiwa muda wa kujiweka tayari.
Hamdi aliyerithi mikoba ya Sead Ramovic ameiongoza Yanga dhidi ya JKT Tanzania ilipotoka suluhu, kisha kushinda 6-1 dhidi ya KenGold na juzi iliizima Singida Black Stars kwa mabao 2-1, amesema bado anahitaji matokeo kwenye kila mchezo, lakini anatamani kuiandaa timu hiyo ili iweze kuwa kwenye ubora zaidi, lakini muda unanibana nafurahi nimekutana na wachezaji wengi bora na wakomavu hivyo situmii nguvu kuwaelekeza.
“Nimeungana na timu katikati ya msimu sio rahisi kwangu kuijenga timu wakati mashindano yanaendelea nafanya kazi niliyonayo ni kuwajenga kimbinu ili tuweze kufikia malengo ambayo watangulizi wangu waliyaweka mwanzoni mwa msimu kwa kusaidiana na viongozi,” amesema Hamdi na kuongeza:
“Kwenye mechi tatu nilizoisimamia timu nimebaini ninaongoza timu yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa na uzoefu kitu ambacho kinanirahisishia kazi licha ya ratiba kubana, tunatarajia kusafiri kesho Ijumaa kuifuata Mashujaa mchezo wetu ujao unaochezwa Jumapili.”
Hamdi amesema kuondoka Ijumaa ni kujipa muda wa kujiweka tayari kutokana na kukutana na timu ambayo inapambana kutafuta matokeo ili iweze kujiweka kwenye nafasi nzuri na wao pia wanapambana kujiimarisha kileleni kwa lengo la kuhakikisha wanamaliza ligi wakiwa hapo.
“Mchezo utakuwa Jumapili safari ni ndefu, lakini timu itatakiwa kupumzika kabla ya kuvaana na Mashujaa ambayo ina kikosi kizuri na imekuwa bora kwenye uwanja wake wa nyumbani kutokana na takwimu hilo halitaondoa malengo yetu ya kuhitaji pointi tatu dhidi ya wenyeji wetu.”