
MASHUJAA bado inapambana na hali yake ikiumiza kichwa juu ya kocha gani impe jukumu la kuisimamia timu hiyo katika mechi saba zilizosalia za Ligi Kuu Bara.
Taarifa mpya ni kuna makocha watano wamesalia kwenda kufanya uamuzi wa mwisho na mmoja wao atakabidhiwa mikoba hiyo iliyoachwa na Mohammed Abdallah ‘Bares’ aliyesitishiwa mkataba wake Februari 26, 2025.
Taarifa kutoka timu hiyo ya Kigoma ni orodha ya mwisho imesalia na makocha watano wote wazawa ambao ni Adolf Rishard, Salum Mayanga, Malale Hamsini, Charles Boniface Mkwasa na Zuberi Katwila.
“Tumebaki na majina hayo matano, viongozi wa juu kabisa wa timu ndio wataamua kwa kuzingatia mengi lakini muhimu ni ubora wake kwenye kuirudishia timu yetu matokeo mazuri,” alisema bosi huyo na kuongeza.
“Hizi mechi zilizosalia ni ngumu, ndiyo maana tunataka kutulia kupata kocha sahihi ili tusifanye makosa ya kimaamuzi yatakayotuvuta chini zaidi.”
Kwenye mechi 10 zilizopita, Mashujaa imeshinda moja pekee ikitoa sare tatu na kupoteza sita ikiwa kwenye nafasi ya 10 na pointi zake 24 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikishika nafasi 10 ikicheza mechi 23.