
WAKATI kaimu kocha mpya wa Mashujaa, Charles Fred akichekelea kuanza vyema kibarua baada ya kuambulia sare ya 2-2 ugenini mbele ya KenGold, mshambuliaji wa timu hiyo, Crispin Ngushi amesema kasi yao inarejea upya baada ya kupoteana katika mechi zilizopita.
Mashujaa ilikuwa na mwanzo mzuri katika msimu huu kabla ya mambo kutibuka na kufikia uamuzi wa kuachana na aliyekuwa kocha mkuu, Mohamed Abdalah ‘Baresi’ kufuatia matokeo yasiyoridhisha.
Kabla ya uamuzi huo, Mashujaa kwenye mechi sita mfululizo, walipoteza mechi nne ikiwa ni dhidi ya Prisons 2-1, Azam 2-0, Yanga 5-0 na Singida BS 3-0, ikishinda moja dhidi ya Pamba 2-0 na sare moja mbele ya Coastal Union.
Fred alianza kibarua chake katika mchezo wa Kombe la Shirikisho kwa kuinyuka Geita Gold iliyopo Ligi ya Championship 1-0 na juzi aliambulia alama moja katika sare ya 2-2 dhidi ya Ken Gold.
Kocha huyo alisema matokeo hayo si mabaya sana, kutokana na ukweli ni siku chache tangu apewe jukumu la kuongoza timu hiyo, akieleza kuridhishwa na kiwango cha nyota wa kikosi hicho.
“Yapo mabadiliko makubwa yanayotoa matumaini, nahitaji kuona tunapambania nafasi tano za juu, Kombe la Shirikisho ni sehemu ya mikakati yetu kufika mbali,” alisema Fred, huku nyota wa timu hiyo, Ngushi aliyewahi kucheza Mbeya Kwanza na Yanga, akitamba kwamba kwa sasa wanarejesha upya makali yao kuhakikisha wanapambania nafasi za juu kwenye msimamo.
“Mpira una matokeo matatu, kuna muda unajipanga kushinda yanatokea mengine, lakini kwa sasa tunaona mabadiliko mazuri na kila mechi kwetu ni fainali ya pointi tatu,” alisema nyota huyo anayemiliki mabao mawili hadi sasa katika Ligi Kuu.
Kwa sasa Mashujaa ipo nafasi ya 10 ikiwa na pointi 24 kupitia mechi 23, ikishinda tano, kutoka sare tisa na kupoteza pia tisa ikifunga mabao 19 na kufungwa 28 na imesaliwa na mechi saba kabla ya kumaliza msimu na mchezo ujao utakuwa dhidi ya Fountain Gate utakaopigwa Aprili 5 mjini Kigoma.