Mashujaa dakika 630 bila ushindi Bara

WAZEE wa Mapigo na Mwendo, Mashujaa ya Kigoma imefikisha dakika 630 bila kuonja ushindi katika Ligi Kuu Bara baada ya juzi jioni ikiwa nyumbani kutoka suluhu na Coasta Union.

Mashujaa inayoshiriki ligi hiyo kwa msimu wa pili mfululizo tangu ilipopanda mwaka juzi, mara ya mwisho kuonja ushindi ilikuwa Novemba 23, mwaka jana ilipoikamua Namungo ya Lindi kwa bao 1-0 mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma ambao ni nyumbani kwa timu hiyo.

Suluhu ya juzi ilikuwa ni sare ya nne kwa Mashujaa katika mechi saba ilizocheza tangu iliposhinda mara ya mwisho, huku michezo mitatu mingine ikipoteza ukiwamo dhidi ya Yanga iliyocharazwa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam.

mechi nyingine mbili ilipoteza mbele ya Dodoma Jiji (1-3) na Tanzania Prisons (1-2) na kuifanya kufikisha pointi 20 kwa sasa kupitia mechi 18, ikishinda michezo minne, sare nane na kupoteza sita, huku ikifunga mabao 15 na kufungwa 16.

Mechi tatu ilizotoka sare ni pamoja na JKT Tanzania, KMC zilizoisha pia kwa suluhu na sare ya 1-1 dhidi ya Kagera Sugar.

Rekodi zinaonyesha katika mechi saba ilizocheza tangu iliposhinda mara ya mwisho, Mashujaa imefunga mabao matano, huku ikiruhusu tisa na kuvuna pointi nne ilhali yenyewe ikipoteza 17, ambapo kikosi kikiwa na sura mpya tatu ikiwamo Emmaneul Martin, Yahya Mbegu na Danny Lyanga walioingia dirisha dogo, huku Ismail Mgunda alichomoka kwenda AS Vita DR Congo.

Pia imeboresha benchi la ufundi kwa kuongeza kocha Charles Fredie kutoka Future Stars Academy ya Arusha, lakini bado vyuma vimekaza na kocha timu hiyo, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ amesema mikakati iliyopo kwa sasa ni kuandaa timu ili mechi zinazokuja wapate ushindi na kurudisha morali kwa wachezaji.

“Hatujawa na mwenendo mzuri, lakini ligi ni ngumu. Kama mwalimu nafanya kila namna kwa kushirikiana na wenzangu ili kila kitu kikae sawa,” alisema Baresi aliyeongeza kuwa timu hiyo ni nzuri licha ya kucheza mechi nyingi mfululizo bila ushindi ila bado anaamini kikosi kina vijana watakaoweza kuwafikisha kwenye malengo waliyojiwekea mwishoni mwa msimu.

Mashujaa imesaliwa na mechi 12 ikiwamo inayopigwa wikiendi hii dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex kabla ya kukabiliana na Pamba Jiji, Yanga, Singida Black Stars, KenGold, Fountain Gate, Tabora United, Namungo, Simba, Kagera Sugar, KMC na JKT Tanzania watakaofunga nao hesabu.

Msimu wa kwanza katika Ligi Kuu, Mashujaa ilipambana dakika za mwisho na kumaliza nafasi ya nane ikiwa na pointi 35 katika mechi 30 baada ya duru la kwanza kuburuza mkia.