
Dar es Salaam. Siku kadhaa baada mwanafunzi wa kidato cha pili, Mhoja Mduhu kufariki dunia kufuatia adhabu ya viboko aliyopewa na mwalimu wake, mashirika yanayopinga ukatili kwa watoto ikiwemo adhabu za kikatili shuleni yameitaka Serikali kuondoa mwongozo wa elimu wa mwaka 2002 juu ya adhabu ya viboko.
Mashirika hayo yametaka pia kuandaliwa kwa mwongozo wa adhabu mbadala na chanya zitakazohimiza nidhamu kwa wanafunzi.
Hata hivyo, kwa upande wa Serikali wamesisitiza kuhusu mwongozo wa adhabu ya viboko kwamba unapaswa kutolewa na mwalimu mkuu au mkuu wa shule na havipaswi kuzidi vitatu.
Mashirika hayo ni Hakielimu, Msichana Initiative, Save the Children, Children Dignity Forum, Shule Direct, Children in Cross Fire, na TCRF.
Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mutahabwa akizungumza na Mwananchi amesema adhabu ya viboko haiwezi kuondolewa kabisa ila linachofanyika wameimarisha ufuatiliaji kuhakikisha adhabu hii inatolewa kulingana na mwongozo.
Tukio la kifo cha Mduhu lilitokea Februari 26, 2025 katika Shule ya Sekondari Mwasamba iliyopo wilaya ya Busega mkoani Simiyu ambapo inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo alifariki dunia baada ya kuchapwa viboko 10 na kukanyagwa kichwani na mwalimu wake aitwaye Salim Chogogwe.
Mwanafunzi huyo alikumbana na adhabu hiyo baada ya kushindwa kufanya kazi za vikundi iliyotolewa na mwalimu huyo, ambapo kwa mujibu wa mmoja wa wanafunzi waliokuwepo eneo la tukio, Maduhu alipigwa fimbo za kichwani na mgongoni kisha kukanyagwa.
Hii si mara ya kwanza kwa tukio la aina hii kutokea, mwaka 2018 mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kibeta iliyopo manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Sperius Eradius alifariki dunia kutokana na adhabu ya viboko kutoka kwa mwalimu wake.
Akizungumza leo Machi 6, 2025 Mkurugenzi wa Shirika la Hakielimu, Dk John Kalage amesema kutokana na kukithiri kwa matukio hayo ni wakati wa Serikali kuchukua hatua za kukomesha matumizi ya viboko shuleni na kuweka mwongozo wa adhabu mbadala, ili kukomesha ukatili kwa wanafunzi.
Dk Kalage amesema katika kipindi hiki ambacho Serikali inafanya mapitio ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 ni muhimu kuweka vipengele vya kuzuia matumizi ya viboko shuleni na adhabu zingine zinazotoa mianya kwa walimu kufanya ukatili kwa wanafunzi.
Amesema ushahidi wa utafiti uliofanywa na Hakielimu katika shule nane umeonyesha kuwa asilimia 98 ya wanafunzi wanajihisi kuwa salama kwa sababu walimu hawatumii adhabu za viboko.
“Serikali inaweza kutumia ushahidi huu kama funzo kuwa matumizi ya adhabu chanya yanawezekana katika kuhimiza nidhamu kwa wanafunzi bila kuwafanyia ukatili. Kuweka sheria ya kupiga marufuku viboko itasaidia kuzuia walimu kutumia adhabu hiyo, hivyo kupunguza na kuondoa ukatili kwa wanafunzi shuleni.
“Pia, tunaitaka Serikali kuweka mpango wa utekelezaji wa ahadi iliyoiweka katika mkutano wa kwanza wa mawaziri wa dunia kuhusu kutokomeza ukatili dhidi ya watoto ulifanyika Novemba, 2024 nchini Colombia, uliotaka kuanzishwa kwa madawati ya ulinzi wa watoto katika shule zote ifikapo mwaka 2029.”
Amesema madawati hayo yatatoa mfumo rasmi wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya watoto wanaokumbwa na ukatili wa aina mbalimbali shuleni ikiwa ni pamoja na vipigo, unyanyasaji wa kijinsia na kisaikolojia.
Kwa upande wake meneja programu wa Shirika la Children in Crossfire, Saraphina Lelo amesema licha ya aina hiyo ya ukatili kufanyika zaidi shuleni, ipo hatari ya kuendelea kutengeneza jamii yenye vitendo vya ukatili.
“Inawezekana haya yanafanyika shuleni, lakini huyu mtoto anakua anaibeba hiyo trauma na ndiyo mfumo wa maisha, ikumbukwe huyu mtoto ndiye atakuja kuwa baba au mama hivyo anaweza kuendeleza adhabu hiyo kwa watoto wake. Jamii itaendelea ikijua viboko ndiyo adhabu sahihi kwa mtoto wakati inamuumiza,” amesema Saraphina.
Akizungumzia suala hilo, Dk Mutahabwa amesema kinachofanywa na Serikali ni kufuatilia kwa ukaribu kuhakikisha mwongozo unatekelezwa kama ulivyotolewa.
Kulingana na mwongozo huo adhabu ya viboko kwa mwanafunzi inapaswa kutolewa na mwalimu mkuu au mkuu wa shule na havipaswi kuzidi vitatu.
“Kusema kwamba adhabu ya viboko itaondoka kabisa sio kweli, hilo linaweza kutokea huko siku za usoni, lakini tunachofanya ni kuimarisha ufuatiliaji kuhakikisha adhabu hii inatolewa kulingana na mwongozo.
“Ufuatiliaji wetu utaongezeka maradufu, watakaokiuka watachukuliwa hatua. Hakuna kitu muhimu kwetu kama usalama wa mtoto hivyo wanajamii tunapaswa kushirikiana kwa kutoa taarifa pale unapofanyika ukatili ili hatua zichukuliwe,” amesema Dk Mutahabwa.
Kamishna huyo ameongeza kuwa ufuatiliaji huo utaenda kuongezeka maradufu kwa wadhibiti ubora wa elimu, akifafanua kwamba wao ndiyo watakuwa wa kwanza kuhojiwa yanapotokea matukio ya ukatili wa wanafunzi shuleni.
“Kama mdhibiti ubora upo na shule yako ina kawaida ya kutoa adhabu kali basi wewe hufai, ni lazima kuwe na ufuatiliaji wa karibu kujua kinachoendelea shuleni.”