Masheha, watendaji walaumiana uchimbaji holela mchanga, mawe

Unguja.  Wakati Wizara ya Maji, Madini na Maliasili Zanzibar ikidai masheha ndio wanawajibika kulinda mali zisizohamishika, wao wamesema baadhi ya watendaji wa wizara ndio wanaoshirikiana na watu wanaofanya uharibifu huo. 

Kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2015, utartibu wa kuchimba mchanga, mawe na kuvisafirisha vinatakiwa kuombewa kibali maalumu wizarani huku yakitengwa maeneo maalumu ya kuchimbwa rasimali hiyo ili kuepusha uharibifu wa mazingira kulingana na uchache wa ardhi yake ilivyo.

Hata hivyo, katika mafunzo yaliyoandaliwa na wizara hiyo kwa masheha wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Aprili 18, 2025 kwa ajili ya kulinda rasimali hiyo, licha ya masheha kudaiwa kuzembea katika ulinzi, wao wamesema watendaji wa wizara ndio wanasababisha jambo hilo kuwa gumu.

Kwa upande wao masheha wa mkoa huo walisema kuwa bado kuna changamoto kubwa juu ya usimamizi wa rasilimali hizo kwani rasilimali hizo huchimbwa usiku katika baadhi ya maeneo bila kuwepo kwa wasimamizi wa rasilimali hizo.

“Baadhi ya watendaji wa wizara ambao sio waaminifu wamekuwa wakishirikiana na wenye magari ya kubebea rasilimali hizo bila ya kufuata taratibu na kuiacha Serikali kukosa mapato yake,” amesema Sheha wa shehia Kiliman Ussi Haji Baro.

Amesema kutokana na hali hiyo imekuwa vigumu kuyakamata magari yanayoiba rasilimali hizo katika shehia zao kwani wanaondoa namba za magari yao.

Amesema masheha wamekuwa mstari wa mbele katika kulinda rasilimali hizo lakini bado kuna changamoto kubwa kwa jamii juu ya kujua umuhimu wa rasilimali hizo kwa kukuza mapata ya taifa.

Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji wa wizara hiyo, Mwanamosi Ali Mwinchande amesema masheha wanao wajibu wa kuzisimamia vizuri maliasili zisizorejesheka ili kuendelea kuwa vyanzo vya kukuza mapato ya taifa. 

Amesema masheha wanadhamana kubwa katika shehiya zao katika kulinda rasilimali hizo zisiaharibiwe ili kuendelea kuwa vyanzo vya mapato kwa serikali. 

“Uhalisia unaonesha nyie masheha ndio wasimamizi wakuu mnapaswa kutambua utaratibu mzima wa utoaji wa vibali vya zasilimali hizo,” amesema Mwanamosi. 

Amesema kuwa kunasheria nyingi zimetungwa juu ya udhibiti wa rasilimali hizo lakini bado kuna baadhi ya wananchi hawazifuati sheria hizo wakati wa kuchimba au hata kusafirisha rasilimali hizo. 

Akitoa mada juu ya utaratibu wa usimamizi wa rasilima hizo mwanasheria wa Wizara hiyo, Nabila Juma Shaaban amesema sheria zipo wazi juu ya atakaye kwenda kinyume na utaratibu ulowekwa.

Kwa mujibu wa sheria anayechimba mchanga bila kibali, tani moja faini yake ni Sh500,000, kuondoa  rasilimali hiyo Sh250000 na kosa la kusafirisha  kwa tani moja bila ya kuwa na kibali faini yake ni Sh150,000.

Kwa mujibu sheria mazingira ya mwaka 2015, kibali cha mchanga kupatikanaji wake ni Sh15,000 kwa tani moja pamoja na upakiaji wake  huku tani moja ya mawe ni Sh6500 kwa mujibu wa sheria iliyopo lakini bado kuna changamoto kwa wananchi kufahamu utaratibu huo hivyo masheha inawajibu wa kuwaelekeza wananchi juu ya jambo hilo. 

“Wananchi hawafahamu utaratibu kwa maana hiyo masheha nyinyi viongozi katika jamii waelekezeni wananchi ili kuondosha changamoto hiyo,” amesema mwanasheria. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *