
RIYADH, SAUDI ARABIA. Mshambuliaji, Jhon Duran amepanga kusafiri kwa maili 600 kila siku kutoka Bahrain hadi kwenye timu yake mpya ya Al-Nassr ya Saudi Pro League.
Staa huyo wa Colombia alijiunga na timu hiyo ya Saudi Arabia kwa ada ya Pauni 70 milioni akitokea Aston Villa mwishoni mwa wiki iliyopita lakini amewaambia mabosi wa Al-Nassr anataka kuishi Bahrain.
Steven Gerrard na Jordan Henderson walikuwa wakiishi Bahrain wakati walipokuwa kwenye kikosi cha Al-Ettifaq ya Saudia. Uwanja wa mazoezi wa Al-Ettifaq, Dammam, upo umbali wa mwendo wa saa moja kwa usafiri wa gari kutoka Bahrain — lakini Al-Nassr ipo nje ya mji wa Riyadh, hivyo ni umbali za zaidi ya maili 300. Usafiri wa ndege kutoka Bahrain hadi Riyadh ni mwendo wa saa moja na dakika 20, hivyo Duran itabidi azoee usafiri wa aina hiyo.
Duran, 21, uamuzi wake wa kutaka kuishi Bahrain ni ili kumpa nafasi mpenzi wake kwenda kwenye kumbi za starehe kitu ambacho Saudi Arabia ni kigumu.
Staa Duran amekubali kujiunga na Al Nassr, ambayo itakwenda kumlipa Pauni 16.7 milioni kwa mwaka.
Mshahara huo ni sawa na Pauni 1.4 milioni kwa mwezi, Pauni 321,000 kwa wiki, Pauni 46,000 kwa siku na Pauni 1900 kwa saa. Mkwanja huo utamwezesha kumudu usafiri wa ndege kwa zaidi ya maili 600 kwenda na kurudi Riyadh akitokea Bahrain.
Duran alijiunga na Aston Villa akitokea Chicago Fire kwenye dirisha la Januari 2023 kwa ada ya Pauni 18 milioni.
Oktoba 2024, Duran alisaini mkataba mpya Aston Villa ambao ungemfanya abaki Villa Park hadi 2030. Na sasa ameondoka Villa Park akiwa amefunga mabao 20 katika mechi 78 alizotumikia kikosi hicho cha kocha Unai Emery.
MGAWANYO WA
MSHAHARA WA
DURAN AL NASSR
-Kwa Mwaka: Pauni 16.7 milioni
-Kwa Mwezi: Pauni 1.4 milioni
-Kwa Wiki: Pauni 321,000
-Kwa Siku: Pauni 46,000
-Kwa Saa: Pauni 1,900
-Kwa Dakika: Pauni 31