Mashariki mwa DRC: Washington yawawekea vikwazo maafisa wa Rwanda na Wakongo wa M23

Marekani imeweka vikwazo vya kifedha dhidi ya James Kabarebe, Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda wa Rwanda, na Lawrence Kanyuka, msemaji wa AFC/M23 (Alliance Fleuve Congo), vuguvugu la kisiasa na kijeshi linaloungwa mkono na Kigali, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Wizara ya Fedha ya Marekani inashutumu waziwazi jukumu la James Kabarebe na Lawrence Kanyuka katika maandalizi na kusonga mbele kundi la waasi lenye silaha la M23, linaloungwa mkono na Rwanda, mashariki mwa DRC.

James Kabarebe, Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda wa Rwanda, anaonyeshwa kuwa na jukumu kuu katika kusaidia M23 na kutoa msaada wa kijeshi. Pia ni jenerali wa zamani katika jeshi la Rwanda. Taarifa ya Wizara ya Feda ya Marekani pia inamhusisha kwa jukumu muhimu katika uchimbaji na biashara ya rasilimali za madini mashariki mwa DRC. Lawrence Kanyuka ni msemaji wa kiraia wa vuguvugu la M23 na Alliance Fleuve Congo. Kwa hivyo, anashutumiwa na Marekani kwa kushiriki kikamilifu katika uvunjifu wa amani mashariki mwa DRC.

Vikwazo hivyo vinajumuisha hasa kuzuiwa kwa mali ya watu hao husika na kampuni zao. Kampuni mbili za Kanyuka zilizoko London na Paris pia zimechukuliwa vikwazo. Kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, kutekwa kwa Goma mwishoni mwa mwezi wa Januari na Bukavu baada ya hapo, pamoja na upanuzi wa haraka wa M23 mashariki mwa DRC, ulisababisha maelfu ya vifo vya raia na raia kulazimika kuhama makazi yao. Kwa kuhofia mzozo wa kikanda, Marekani inataka kurejea kwa mazungumzo na kuheshimu ukamilifu wa eneo la DRC.

Kinshasa yakaribisha vikwazo vya Marekani

Kupitia kwa msemaji wake Yolande Makolo, serikali ya Rwanda awali ilielezea uamuzi wa Marekani kama “usio na haki”, ikitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa “kuunga mkono, na sio kudhoofisha, juhudi zinazoendelea za kikanda kwa ajili ya ufumbuzi wa kisiasa”. Baadaye, mkuu wa diplomasia ya Rwanda, Olivier Nduhungirehe, ameelezea maskitiko yake kwamba “badala ya kuchukulia vikwazo makundi haramu yenye silaha […] yanayotumiwa na Rais Tshisekedi, Wizaraya Fedha ya Marekani imechagua kumuwekea vikwazo waziri wa Rwanda […]. “Ni aibu na nadhani kwamba hatua hizi za jumuiya ya kimataifa na Marekani haziwezi kuendeleza amani,” ameripoti mwandishi wa RFI mjini Kigali, Lucie Mouillaud.

“Vitisho vyote vya Magharibi havituathiri zaidi ya hapo: kilicho muhimu kwetu ni kujikinga na vitisho kwenye mpaka wetu”, amesema Olivier Nduhungirehe, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda

Kinshasa, kwa upande wake, imefurahishwa na hatua ya Marekani. Ofisi ya rais wa Kongo, inasema vikwazo hivi vinathibitisha kile ambacho DRC imekuwa ikisema siku zote, yaani kwamba serikali ya Rwanda inahusika na uasi huu wa M23. Imeongeza pia kuwa inatumai kuwa vikwazo hivi ni hatua ya kwanza tu, ikisema kwamba haielewi matakwa ya Umoja wa Ulaya kuhusu suala hili.

“Hii ni hatua ya kwanza ya kukaribisha, lakini tunatumai itaenda mbali zaidi” , amesema Tina Salama, msemaji wa Rais wa Kongo Felix Tshisekedi.