Mashariki mwa DRC: Wapiganaji wa M23 wanaendelea kusonga mbele Kivu Kaskazini na Kusini

Likiungwa mkono na jeshi la Rwanda, kundi hilo lenye silaha la M23 linaendelea kupata nguvu katika mikoa miwili ya mashariki mwa DRC. Huko Kivu Kusini, kusonga mbele kwa M23 kumesababisha hali ya hofu na uporaji katika mji wa Uvira, mji ulio kwenye mpaka na Burundi ambapo wakaazi pia wameripoti mapigano kati ya wanajeshi wa Kongo na wanamgambo wa Wazalendo kwa siku kadhaa. Katika siku nzima ya Alhamisi, Februari 20, mapigano pia yaliripotiwa katika maeneo kadhaa.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Na mwanahabari wetu mjini Kinshasa, Coralie Pierret

Kusonga mbele kwa M23, wakiungwa mkono na jeshi la Rwanda, kuliendelea katika miko miwili ya Kivu, siku ya Alhamisi hii, Februari 20.

Kwanza, huko Kivu Kaskazini, mapigano yamezuka tena katika maeneo kadhaa huko Lubero ambapo hali imekuwa mbaya kwa siku kadhaa. Kundi hilo lenye silaha na washirika wake wanaendelea kusonga mbele kwenye barabara ya taifa nambari 2 kuelekea Butembo na Beni, miji miwili muhimu kaskazini mwa mkoa huo.

Katika sehemu yake ya kusini, magharibi mwa Goma, huko Masisi, wanajeshi wa Kongo wanaoshirikiana na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali, Wazalendo, walipambana na wapiganaji wa M23. Mapigano hayo yalimjeruhi vibaya mfanyakazi wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) aliyepigwa risasi akiwa ndani ya kituo cha shirika hilo mkoani humo. Mtoto ambaye alikuwa amekimbilia katika kituo hiki pia alipigwa risasi.

Sintofahamu katika uwanda wa Ruzizi

Huko Kivu Kusini, siku tatu baada ya M23 kuteka mji wa Kamanyola siku ya Jumanne, Februari 18, sntofahamu ilitawala siku ya Alhamisi, Februari 20, kando ya barabara ya taifa nambari 5, inayojulikana pia kama uwanda wa Ruzizi, bonde linalofuata mpaka kati ya DRC na Burundi.

Huko Uvira, mji wa pili katika mkoa huo ulioko kilomita 75 kusini mwa Kamanyola, mapigano yaliripotiwa kati ya wanajeshi wa Kongo na wanamgambo wa Wazalendo, pamoja na uporaji, haswa katika nyumba ya mchungaji katikati mwa jiji na nyumba za watu binafsi, kulingana na wakaazi wa eneo hilo. Mmoja wao anasimulia kuwa aliona “watu wenye silaha” wakiwemo wanajeshi wa Kongo au washirika wao, ambao “walitoroka Bukavu”, mji mkuu wa Kivu Kusini ambao M23 waliuteka mwishoni mwa juma lililopita.

“Baadhi yao kwanza walibomoa mlango wa nyumba yangu. Kisha walifika kwa wingi kuchukua maharage, mchele na vyakula,” shahidi huyo ameongeza.

Kulingana na chanzo cha misaada ya kibinadamu, ghasia zilizotokea mjini Uvira zimesababisha vifo vya watu kadhaa na majeruhi kadhaa. Pia vurugu hizi zimesababisha wakazi wengi kukimbilia kusini au nchi jirani ya Burundi. Likiwasiliana na RFI, jeshi la Kongo lilikiri kuwepo kwa “urushianaji risasi huko Uvira” lakini likabainisha kwamba  “hali haikuzorota katika mji huo”.