Mashariki mwa DRC: Umoja wa Mataifa washutumu M23 kwa kuua watoto Bukavu

Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne, Februari 18, umeshutumu kundi la wapiganaji la M23, ambalo wapiganaji wake wanaoshirikiana na wanajeshi wa Rwanda wameudhibiti mji wa Bukavu mashariki mwa DRC, kwa kuwaua watoto.

Imechapishwa:

Dakika 2

Na: RFI na mashirika mengine

Matangazo ya kibiashara

Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imethibitisha kesi za mauaji ya watoto wiki iliyopita huko Bukavu, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Hali “inazidi kuzorota,” msemaji wa ofisi hiyo huko Geneva amesema siku ya Jumanne.

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu “amethibitisha kesi mauaji ya watoto yalitekelezwa na M23 baada ya kuingia katika mji wa Bukavu wiki iliyopita,” na “tunatoa wito kwa Rwanda na M23 kuhakikisha kuwa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu zinaheshimiwa,” msemaji wa Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani amesema, wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Umoja wa Mataifa unajua kuwa watoto wanamiliki silaha, amewaambia waandishi wa habari. “Hatuna idadi kamili” ya mauaji kwa sababu hali ni tete, ameongeza. Anataja watoto watatu waliouawa siku ya Jumapili iliyopita huko Bukavu walipokuwa wakikusanya silaha katika maeneo yaliyotelekezwa na jeshi la Kongo. “Waliamriwa kuweka chini silaha zao. Walikataa na wakauawa,” msemaji huyo ameongeza.

Kamishna Mkuu anatoa wito kwa Rwanda na M23 kuheshimu haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu (IHL). Ameandika ukiukaji, unyanyasaji wa kijinsia na vitisho.

Amepata taarifa za watu kukamatwa kiholela na kuwekwa kizuizini. Pamoja na shutuma za kurejea kwa lazima kwa vijana wa Kongo waliokimbia ghasia katika nchi jirani.

Umoja wa Mataifa pia umepokea maombi ya ulinzi kutoka kwa waathiriwa na mashahidi wa ukiukaji wa haki za binadamu kufuatia maasi siku chache zilizopita kutoka kwa magereza kadhaa ambapo wafungwa walitoroka. Kamishna Mkuu Volker Türk anatoa wito kwa Rwanda na M23 kuhakikisha ulinzi wa watu wote.

Kwa upande wake, shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (HCR) limesema kuwa kati ya watu 10,000 na 15,000 wamefika Burundi katika siku za hivi karibuni, hasa kutoka mkoa wa Kivu Kusini. Mashariki mwa DRC, karibu watu 350,000 hawana makazi.

Ghasia za wiki za hivi karibuni ambazo zilisababisha kutekwa kwa mji wa Goma na waasi wa M23 zimeacha karibu waathiriwa 3,000, kulingana na Umoja wa Mataifa na mamlaka ya Kongo. Maelfu ya watu pia walijeruhiwa.