
Rais wa DRC Félix Tshisekedi amefanya ziara nchini Angola siku Jumanne 18 Februari kukutana na mwenzake wa Angola João Lourenço, ambaye ni rais wa sasa wa Umoja wa Afrika. Mkutano huu unakuja siku tatu baada ya waasi wa AFC/M23 wakiungwa mkono na jeshi la Rwanda RDF, kuuteka mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kusini, Bukavu.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Majadiliano kati ya Félix Tshisekedi na Joao Lourenço yalilenga maendeleo ya AFC/M23, hasa katika mkoa wa Kivu Kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Kwa upande wa kidiplomasia, hakuna maendeleo makubwa yaliyopatikana. Wakuu hao wawili wa nchi walijadili hatua zinazopaswa kuchukuliwa, katika ngazi ya nchi mbili na kikanda.
Pia walijadili mahitimisho ya mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, uliofanyika siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita mjini Addis Ababa. Umoja wa Afrika hautaja wala kulaani Rwanda, ukisisitiza kutokuwepo kwa suluhisho la kijeshi kwa mzozo huo na kutaka diplomasia na mazungumzo yapewe kipaumbele. Baraza la Umoja huo lilihimiza kuanzishwa tena mara moja kwa mazungumzo na washikadau wote, ikiwa ni pamoja na M23, ndani ya mfumo wa mchakato wa Luanda na Nairobi.
Kulingana na vyanzo kadhaa, Angola inaunga mkono mbinu hii ya mazungumzo. Félix Tshisekedi, kwa upande mwingine, anakataa mazungumzo yoyote ya moja kwa moja na M23 na anasisitiza juu ya kuanzishwa upya kwa mchakato wa Luanda, ambao unahusisha moja kwa moja Kigali. Katika hatua hii, hakuna maelezo yoyote ambayo yametolewa juu ya hitimisho la majadiliano yao.
Kwa upande wake, jumuiya ya kimataifa inategemea ukaribu kati ya Joao Lourenço na Félix Tshisekedi ili kupunguza mgogoro huo. Ziara hii inajiri baada ya rais wa Kongo kuwa tayari amesafiri hadi Luanda takriban wiki tatu zilizopita kwa mkutano mwingine na mwenzake wa Angola.