
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy ametangaza siku Jumanne, Februari 25, kwamba Uingereza itasitisha misaada yake mingi kwa Rwanda “hadi maendeleo makubwa yatakapopatikana.” London inashutumu kutekwa kwa Goma na Bukavu na “M23 na vikosi vya ulinzi vya Rwanda”.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
“Uhasama lazima ukome mara moja. “Mashambulizi ya hivi majuzi ya M23 na vikosi vya ulinzi vya Rwanda, na haswa kutekwa kwa Goma na Bukavu, ni ukiukaji usiokubalika wa uhuru na uadilifu wa eneo la DRC,” Ofisi ya Mambo ya Nje imesisitiza katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Fedha hizi zitasitishwa “kwa kukosekana kwa maendeleo makubwa”, isipokuwa programu za Uingereza kwa raia nchini Rwanda. London pia imesema inapanga “kuratibu na washirika juu ya uwezekano wa vikwazo vipya.” Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy alikutana na Rais wa DRC Félix Tshisekedi mjini Kinshasa na Rais wa Rwanda Paul Kagame mjini Kigali Februari 21 na 22.
Kusitishwa huko kunahusu nyanja kadhaa kama vile msaada wa moja kwa moja wa fedha baina ya nchi mbili kwa serikali ya Rwanda, mafunzo ya kijeshi na shughuli za kukuza biashara na Rwanda. Programu tu zinazolenga “maskini zaidi na walio hatarini zaidi” ndizo zitatekelezwa.
Uamuzi unaochukuliwa kuwa “wa kusikitisha na usio na busara” na serikali ya Rwanda, ambayo inadai kwamba London “imechagua wazi upande wake” katika mzozo huo, kulingana na mwandishi wetu wa Kigali, Lucie Mouillaud. Hatua za adhabu zilizotangazwa na London ni za “kusikitisha” kwa Kigali, ambayo inatangaza kwamba “hazisaidii DRC kwa njia yoyote” na “hazichangii katika kutafuta suluhu la kudumu la kisiasa”. “Si jambo la busara kutarajia Rwanda kuhatarisha usalama wake na wa Wanyarwanda,” ilmeongeza taarifa hiyo na kuongeza kuwa nchi hiyo itaendelea kudai dhamana katika suala hili.
Hatu hiyo ya Uingereza inakuja chini ya wiki moja baada ya Wizara ya Fedha ya Marekani kuamua kumuwekea vikwazo Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda James Kabarebe, aliyewasilishwa kama mhusika mkuu katika uungaji mkono wa Kigali kwa kundi la waasi la M23. Kiongozi wa kihistoria katika vyombo vya usalama vya Rwanda, jenerali huyo mstaafu alikashifu siku ya Jumanne, wakati wa mkutano na vyama vya siasa, hatua za adhabu dhidi ya Rwanda, ambayo kulingana naye, zinahatarisha juhudi za amani zinazofanywa ndani ya mchakato wa mazungumzo uliounganishwa wa Luanda na Nairobi.
Mwisho wa ushirikiano kati ya London na Kigali?
Mwishoni mwa mwezi wa Januari, David Lammy alitishia Kigali, akionya kwamba mikataba ambayo inaziunganisha nchi hizo mbili inaweza kuangaliwa upya. Kwa hiyo tishio lililotekelezwa baada ya ziara yake huko Kinshasa na Kigali mnamo tarehe 21 na 22 Februari, ambapo waziri wa Uingereza alisisitiza kwamba hakuwezi kuwa na suluhu la kijeshi kwa vita hivi na kwamba taratibu za amani zinazoendelea ndizo njia pekee zinazowezekana.
Kwa hivyo huu unaweza kuwa mwisho wa ushirikiano kati ya London na Kigali? Hadi Julai 2024, Rwanda na Uingereza zilikuwa na uhusiano mzuri sana. Nchi hizo mbili zilikuwa zimehitimisha makubaliano, ambayo yaliruhusu kutumwa kwa wahamiaji haramu katika ardhi ya Uingereza nchini Rwanda. Makubaliano yaliyositishwa na serikali mpya ya Uingereza, ambayo Uingereza ilikuwa tayari imelipa euro milioni 280.