Mashariki mwa DRC: Kundi la AFC/M23 linatishia kuzindua upya operesheni zake kijeshi

Vuguvugu la waasi la AFC/M2 katika taarifa yake ya Aprili 10, 2025, limetishia kuanzisha upya operesheni zake za kijeshi. Vuguvugu hilo linashutumu Wanajeshi wa DRC (FARDC) kwa kukiuka usitshwaji mapigano ambao ulionekana kuwa katika harakati za kuanzishwa, haswa baada ya kujiondoa kwa kundi hili kutoka eneo la Walikale-centre, wiki moja iliyopita.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

AFC/M23 inatangaza nia yake, inasema, kuondoa tishio lolote dhidi mchakato huo. Kauli hii inajiri huku mazungumzo ya amani yakiendelea mjini Doha, yakiwaleta pamoja wajumbe kutoka Kinshasa na AFC/M23. Ni nini kinafafanua tangazo hili, wakati majadiliano yanaendelea? 

Taarifa hii ya AFC/M23 inaweza kuelezewa kwanza na hali ilivyo katika uwanja wa vita, ambapo mapigano yamekuwa yakiendelea kwa angalau siku tatu, hasa katika mkoa wa Kivu Kusini, mashariki mwa DRC.

Katika eneo la Kalehe, vyanzo kadhaa vya ndani vinaripoti mashambulizi ya Wazalendo, wapiganaji wanaounga mkono FARDC, ambao wamefanikiwa kuteka angalau vijiji vinane.

Katika maeneo haya na baadhi ya vijiji vingine, AFC/M23 haikuwa imedumisha uwepo wa kudumu wa wapiganaji wake.

Mnamo Aprili 10, 2025, mapigano mapya yalizuka, haswa katika vijiji vya Bushaku 1 na 2, ambapo Wazalendo walidhibiti vijiji hivi baada ya mapigano makali. Katika eneo hili, Wazalendo ndio wanaoneka na sio FARDC.

Hali kama hiyo ilionekana katika eneo la Kabare, katika mkoa wa Kivu Kusini, karibu na Mbuga ya Kitaifa ya Kahuzi-Biega, ambapo mapigano yaliripotiwa siku ya Alhamisi huko Tshivanga na Mutaka.

Mapigano mengine pia yaliripotiwa katika eneo la Masisi katika siku za hivi karibuni, na kuongeza hali ya wasiwasi.

“Kutokuaminiana” wakati wa mazungumzo nchini Qatar

Sababu nyingine inayoelezea tishio hili la kuanzishwa upya kwa operesheni za kijeshi za AFC/M23 inaweza kuhusishwa na mvutano wa sasa huko Doha, ambapo mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Kongo na AFC/M23 yanafanyika. Ni vigumu kupata taarifa zahihi kuhusu maendeleo ya majadiliano, kwani wapatanishi wanasisitiza juu ya kuwepo kwa usiri mkubwa. Wajumbe wote kutpka pande mbili husika bado wamekwama katika hatua ya utangulizi, wakiwa na majibu machache thabiti kuhusu hatua za kujenga imani zitakazowekwa kabla ya kushughulikia masuala muhimu. Hili linathibitishwa na chanzo cha kidiplomasia ambacho kinaeleza kuwa majadiliano bado yanakumbwa na hali ya “kutokuaminiana.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *