
Siku ya Alhamisi tarehe 13 Februari, wabunge wa Umoja wa Ulaya waliokutana huko Strasbourg karibu kwa kauli moja wametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mkataba uliotiwa saini Februari 2024 na Rwanda.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Mkataba huo ambao ulikosolewa vikali na DRC, unasalia kuwa kizingiti cha mvutano kati ya Kinshasa na taasisi hiyo ya Ulaya, ambayo, baada ya kukamilika kwa mktaba huo, ulishutumiwa kwa kuhimiza “uporaji wa maliasili ya Kongo unaofanywa na Rwanda.” Wiki iliyopita, mamlaka huko Kinshasa iliomba kufutwa kwa mkataba huo. Na wabunge kwa hiyo wamethibitisha kuwa ni sahihi.
Azimio hilo limepitishwa kwa kura 443 za ‘Ndio”, na kura nne pekee zinazopinga. Kupitishwa kwa azimio hilo ni “ushindi” anasema mbunge Marc Botenga, ambaye amekuwa akifanya kampeni kwa karibu mwaka mzima ili mkataba huo usitishwe, na ni mwandishi wa azimio lililopendekezwa.
“Nadhani changamoto ni kutumia azimio hili kuweka shinikizo kwa Tume ya Ulaya kwa kusema kwamba, kwa sera yako, hakuna tena mamlaka ya kidemokrasia. Na kuitumia kwa kiwango cha kitaifa, kuziambia serikali za kitaifa na mabunge ambayo hayajachukua hatua dhidi ya ukiukaji huu wa sheria za kimataifa, kuwaambia “chukuweni hatua” ili msihusiki katika vita vilivyodumu kwa karibu miongo mitatu. “
Alipoulizwa na shirika la habari la AFP, Mounir Satouri, mbunge kutoka kundi la Kijani na rais wa kamati ya haki za binadamu, anazingatia kwamba “ushirikiano wa kimkakati wa Umoja wa Ulaya, EU, na Rwanda katika sekta ya malighafi endelevu haukuweza kutetewa tangu mwanzo”.
Uchimbaji madini katika eneo la Kongo umethibitishwa na Umoja wa Mataifa. Kulingana na kundi la wataalam, waasi wa M23 hukusanya karibu dola 800,000 kwa mwezi kutoka kwa ushuru wa biashara na usafirishaji wa madini adimu kuelekea Rwanda.
Mbali na ombi la kusitishwa mara moja kwa Mkataba wa Maelewano, azimio hilo linaitaka Tume hiyo “kuzuia msaada wa moja kwa moja wa kibajeti kwa Rwanda hadi itakapotimiza masharti yanayohusiana na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu na kukata uhusiano na M23” pamoja na “kuzuia msaada wa kijeshi na usalama kwa jeshi la Rwanda”.
Kwa mujibu wa habari zetu, vikwazo dhidi ya vigogo katika jeshi la Rwanda pia viko mezani, japo vitambulisho vyao havijulikani.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Maxime Prévôt, ametoa wito wa vikwazo dhidi ya Rwanda, akizungumza na mwandishi wetu wa habari huko Brussels, Pierre Benazet.
Euro milioni 900 zilizotengwa kwa Rwanda mnamo 2023
Je! Tume ya Ulaya itaamua kuzuia fedha hizi? Kigali inasalia kuwa mmoja wa washirika waliobahatika wa EU katika bara la Afrika. Mnamo Desemba 2023, Umoja wa Ulaya ulitangaza kuwa, kama sehemu ya mpango wake wa maendeleo wa Global Gateway, zaidi ya Euro milioni 900 zitatengwa kwa Rwanda. Mnamo Novemba 2024, euro milioni 20 pia zilitolewa kwa jeshi la Rwanda, lililotumwa kaskazini mwa Msumbiji kudhibiti waasi wa kijihadi katika eneo ambalo kampuni ya Ufaransa ya TotalEnergies imejengwa na inafanya kazi.
Katika mahojiano yaliyorushwa na Jeune Afrique siku ya Jumatano, Rais wa Rwanda Paul Kagame alionya kwamba “kati ya kukabiliwa na tishio lililopo na kukabiliwa na vitisho vya kuadhibiwa na vikwazo vya nje, bila kusita, ninalenga silaha zangu kwenye tishio lililopo.”