San’aa. Shambulizi lililolofanywa kwa ndege ya kijeshi ya Marekani nchini Yemen limesabababisha vifo vya watu wanne huku kadhaa wakijeruhiwa.
Al Jazeera imeripoti leo Jumatano Aprili 2, 2025, kuwa watu wanne waliouawa ni waliokubwa na shambulizi lililotokea eneo la Hodeidah nchini Yemen, ikiwa ni mwendelezo wa mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya vikosi vya Wahouthi nchini humo.
Marekani pia inatajwa kupeleka meli kubwa ya pili kwa ajili ya kubeba ndege za kijeshi zitakazotumika kurusha makombora na kutekeleza mashambulizi ya kijeshi eneo la Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Waziri wa Afya wa Wahouthi, Anees Alasbahi, watu watatu wamethibitishwa kuuawa katika shambulizi la Marekani lililotekelezwa Jumanne usiku lakini idadi hiyo imeongezeka asubuhi ya leo Jumatano na kufikia watu watano.
“Shambulizi la Marekani, ambalo lililenga jengo la usimamizi wa maji katika Wilaya ya al-Mansouriyah katika Jimbo la Hodeidah kwa mashambulizi kadhaa Jumanne, limesababisha vifo vya watu wanne na majeruhi wawili, ambao wengi wao ni wafanyakazi,” amesema Alasbahi.
Runinga ya Al Masirah, inayohusiana na Wahouthi, imeripoti kuwa eneo la Hajjah lililopo Kaskazini-Magharibi na Saada kaskazini pia yalishambuliwa.

Meli ya Marekani inayobeba ndege za kijeshi zinazotekeleza mashambulizi Yemen dhidi ya Wahouthi.
Marekani haijathibitisha kuwa ilifanya mashambulizi hayo, ambayo yalitokea baada ya Al Masirah kuripoti mashambulizi kadhaa ya Marekani kwenye maeneo ya Saada na Sanaa.
Pia hakukuwa na ripoti za haraka kuhusu vifo kutokana na mashambulizi ya Jumatatu usiku.
Zaidi ya watu 60 wameuawa Yemen tangu Marekani ilipoanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Wahouthi mnamo Machi 15.
Kundi hilo la wapiganaji wa Kihouthi lilikuwa limetishia kurejesha mashambulizi dhidi ya meli zinazohusiana na Israeli katika Bahari Nyekundu kufuatia uvunjwaji wa sitisho la mapigano huko Gaza.
Pentagon pia imetangaza kuwa itaongeza idadi ya meli zake za kubeba ndege katika ukanda wa Mashariki ya Kati hadi kufikia mbili, ikihifadhi moja iliyoko Bahari Nyekundu na kupeleka nyingine kutoka eneo la Asia-Pasifiki.
Meli ya USS Carl Vinson itaungana na USS Harry S Truman katika eneo la Mashariki ya Kati, Pentagon ilisema katika taarifa yake ya Jumanne, ikiongeza kuwa Marekani pia itapeleka ndege zaidi za kijeshi.
“Marekani na washirika wake wanabaki kujitolea kwa usalama wa kanda katika eneo la CENTCOM (Eneo la Majukumu ya Amri ya Kati) na wako tayari kujibu hatua zozote za Serikali au makundi yasiyo ya kiserikali yanayotaka kuchochea mgogoro katika eneo hilo,” Pentagon ilisema.
Vikosi vya Wahouthi pia vilidai Jumanne usiku kuwa vilirusha makombora kadhaa ya masafa marefu na droni dhidi ya meli za Marekani katika kundi la meli la USS Truman, huku wakisema wamefanikiwa kudungua ndege isiyo na rubani (droni) ya Marekani.

Ilikuwa ni shambulizi la tatu dhidi ya vyombo vya kijeshi vya Marekani ndani ya saa 24, Wahouthi walisema katika taarifa iliyotangazwa na Al Masirah TV.
Ingawa Pentagon haikutaja aina ya ndege zinazotumwa eneo hilo, maofisa wa Marekani waliiambia Shirika la Habari la Reuters kwa masharti ya kutotajwa majina kuwa angalau ndege nne za kivita za B-2 zimehamishiwa katika kituo cha kijeshi cha Marekani na Uingereza kilicho katika Kisiwa cha Diego Garcia kilichopo ndani ya Bahari ya Hindi.
Kulingana na wataalamu, kituo cha Diego Garcia kiko ndani ya eneo linaloweza kufikiwa na makombora ya Yemen na Iran.
Kitengo cha Mipango cha Jeshi la Marekani kimekataa kusema ni ndege ngapi za B-2 zimefika katika Kisiwa cha Diego Garcia na kimesisitiza kuwa hakitoi maoni kuhusu mazoezi ama operesheni zinazohusisha ndege hizo.
Kupelekwa kwa ndege ya pili ya kubeba ndege na mabomu ya B-2 ambayo yapo 20 pekee katika orodha ya Jeshi la Anga la Marekani na hutumiwa kwa tahadhari kunakuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema kuwa mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa Wahouthi yataendelea hadi pale watakapoacha kuwa tishio kwa usafiri wa majini.
Trump pia ameongeza ukali wa matamshi dhidi ya Iran, akitishia Jumapili kuwa kutakuwa na mashambulizi ya mabomu ikiwa Iran haitafikia makubaliano na Washington kuhusu mpango wake wa nyuklia kwa masharti yake.
Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, alisema Jumatatu kuwa Marekani itapata pigo kali ikiwa Trump atatekeleza vitisho vyake.
Kamanda wa Kikosi cha Walinzi wa Anga wa Dola la Kiislamu la Iran, Amirali Hajizadeh, ameionya Marekani kuwa isisahau kuwa ina vituo vya kijeshi Mashariki ya Kati, hivyo kuishambulia Iran na washirika wake ni sawa na mtu anayemiliki nyumba ya vioo huku akianzisha ugomvi kwa kurusha mawe.
Gazeti la Tehran Times pia linaripoti kuwa vikosi vya Iran vimeweka tayari makombora yenye uwezo wa kushambulia maeneo yanayohusiana na Marekani kutokana na vitisho hivyo vya Trump.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.