Mashambulizi Israel yaua 85 Gaza, Ulaya yailima vikwazo

Mashambulizi Israel yaua 85 Gaza, Ulaya yailima vikwazo

Khan Younis. Mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vya Jeshi la Israel (IDF) yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 85 eneo la ukanda wa Gaza katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Shirika la Habari la Associated Press limeripoti leo Jumtano Mei 21, 2025, kuwa mashambulizi hayo yamefanyika maeneo mbalimbali ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya eneo la Gaza, kati ya waathiriwa ni zaidi ya watu 22 waliouawa baada ya IDF kulenga nyumba ya makazi na shule iliyoko eneo la Deir al-Balah huku Israel ikitoa taarifa kuwa ililenga kituo cha kutolea amri cha kundi la Hamas.

Katika shambulizi la aina hiyo lililotekelezwa Deir al-Balah, watu 13 wameuawa usiku wa kuamkia leo baada ya kombora kupiga eneo lenye mahema ya wakimbizi la Nuseirat.

Pia, Hospitali ya Nasser imedai kuwa kuna mashambulizi mawili ya IDF yaliyolenga eneo la Khan Younis na kuua watu 10 ambapo Israel imetoa taarifa na kuishutumu Hamas kwa kuendesha shughuli zake eneo la makazi.

Waziri wa Israel, Benjamin Netanyahu akizungumzia mashambulizi hayo amesema operesheni zake zimerejea baada ya mazungumzo ya Amani kati yao na Hamas kugonga mwamba, huku akisema anaamini awamu nyingine inaweza kurejesha amani katika eneo hilo.

Kati Netanyahu akitoa kauli hiyo, baada ya watu wamekosoa uamuzi wake wa kuamuru mashambulizi yarejeshwe eneo la Gaza, huku Yair Golan ambaye ni Jenerali mstaafu wa Israel amemkosoa vikali.

Golan amesema kitendo cha IDF kutekeleza mashambulizi yake kwa kulenga makazi ya watu na kuwaua watoto na wanawake ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa na haki za binadamu.

‘Taifa linalojitambua haliwezi kutekeleza mauaji ya raia na watoto kama sifa hata bila kutoa taarifa kwa raia kuondoka maeneo ya hatari kabla ya kutekeleza mashambulizi yake,” amesema Golan.

Baada ya kauli hiyo ya Golan, Netanyahu aliibuka na kumjibu kupitia kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii na kudai kuwa siyo kauli inayopaswa kuzungumzwa na kiongozi wa umma na kudokeza kuwa inalenga kuwatetea magaidi.

Wakati hayo yakiendelea, Waziri Mkuu wa Qatar ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Mohammed bin Abdulrahman Al Thani amedokeza kuhusu mazungumzo ya Amani kati ya pande hizo kuwa hakuna pendekezo lililoonekana kukubaliwa na upande wowote katika mzozo huo.

Hamas nayo imeibuka na kudai kuwa hakuna ofisa yoyote wa Israel ambaye amefika Doha nchini Qatar akiwa na pendekezo lenye nia ya kukomesha vita hiyo huku ikimshutumu Netanyahu kwa kuupotosha jamii ya kimataifa kuhusu mzozo huo.

“Anachokifanya Netanyahu ni maigizo yenye lengo la kuionyesha dunia kuwa anania ya kufikia makubaliano ya kusitisha vita lakini ukweli ni kwamba halengi kufanya hivyo wala hachukua hatua zozote kufikia lengo hilo. Anachotaka ni kuendelea kuwaua watoto na raia wasiyo na hatia,” imesema Hamas.

Katika hatua nyingine, Uingereza imetangaza kusitisha mazungumzo yote ya kibiashara na Israel na kutangaza kuwawekea vikwazo raia watatu wa Israel ambao ni wafanyabiashara wanaoishi eneo la Ukingo wa Magharibi akiwemo, Daniella Weiss, kwa kile inachotaja kuwa ni kupingana na mauaji yanayoendelea eneo la Gaza.

Uamuzi huo umekuja siku moja tangu Ufaransa na Canada kutangaza kusitisha ushirikiano na Israel katika kile kinachotajwa ni kulaani mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu unaotekelezwa na Israel eneo la Gaza kwa kisingizio cha kuwasaka wapiganaji wa Hamas.

“Naomba kuweka wazi hili kwamba tumeshtushwa na kusikitishwa sana na mauaji ya raia wasiyo na hatia eneo la Gaza,” amesema Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Stamer.

Uamuzi huo wa mataifa ya Ulaya ulikosolewa vikali na Serikali ya Israel, kupitia kwa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Oren Marmorstein, ambapo imesema vikwazo hivyo havijazingatia misingi ya haki na usawa kwa kusikiliza pande zote za mzozo.

Misaada kiduchu yaingia Gaza

Umoja wa Mataifa (UN) umesema, baada ya miezi mitatu ya kuzuiwa mpakani, hatimaye juzi magari yenye shehena ya misaada ya kibinadamu yaliruhusiwa kuingia eneo la Gaza japo kwa uchache.

UN imesema baada ya kuongezewa msukumo, Israel wiki hii imeridhia kuruhusu malori machache yenye misaada ya kibinadamu kuingia Gaza ili kunusuru maisha ya watoto yaliyoko hatarini kutokana na tishio la njaa na afya duni.

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric amesema pamoja na kuwa misaada hiyo kuingia eneo la Gaza, watumishi wake wameshindwa kuifikisha maeneo inapohitajika zaidi kwa kile alichodai ni kuwepo amri za IDF kuwataka waihamishie kwenye magari tofauti na yale yaliyoifikisha Gaza.

Pamoja na Shirika la COGAT kudai kuwa malori matano yaliingia Gaza Jumatatu na mengine 93 yaliingia Jumanne, Dujarric amekanusha na kudai kuwa ni malori machache yaliyoruhusiwa kuingia tofauti na inavyodaiwa na COGAT.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, eneo la Gaza tangu kuanzisha mashambulizi yake, Israel imewaua wapalestina zaidi ya 53, 000 na kujeruhi zaidi ya 110,000 huku Hamas ikiwaua Waisrael zaidi ya 1,200 na kuwachukua mateka 251.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *