Mashambulio na mauaji ya kinyama ya Israel yaigeuza Bait Lahia, Ghaza eneo la ‘maafa yasiyoelezeka’

Mamlaka za Palestina katika eneo la Beit Lahia kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza leo zimeutangaza mji huo kuwa “eneo la maafa” wakati jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel linaendelea na mashambulizi yake ya kinyama na mauaji ya kimbari katika eneo hilo la Palestina.

Tamko hilo limetolewa baada ya Wizara ya Afya ya Ghaza kutangaza kuwa Wapalestina wengine wasiopungua 93 wameuawa shahidi na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika shambulio la jeshi la Kizayuni lililolenga jengo la makazi huko Beit Lahia siku ya Jumanne.

Manispaa ya mji huo imesema wakazi wa hapo wanakabiliwa na “janga la kibinadamu,” kutokana na “vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelea sambamba na kuzingirwa mji huo.”

Imeongeza kuwa Beit Lahia sasa haina chakula, maji, hospitali, ambulensi, ulinzi wa raia, usafi wa mazingira wala huduma za mawasiliano.

Ikizindua ombi la dharura la kusaidia “kuokoa kile kinachoweza kuokolewa katika mji huo ambao unakabiliwa na mauaji ya kimbari na maangamizi ya kizazi,” manispaa hiyo imeitaka jamii ya kimataifa na mashirika mbalimbali yaishinikize Israel kukomesha mashambulizi yake na kuruhusu kuingizwa misaada ya kibinadamu, mafuta, ulinzi wa raia, vifaa, na magari ya kusaidia kufungua barabara na kuondoa kifusi.

Hali ya maafa nje ya Hospitali ya Kamal Adwan, kaskazini ya Ghaza

Siku ya Jumanne, zaidi ya Wapalestina 100, wengi wao wakiwa wanawake na watoto waliuawa huko Beit Lahia katika mashambulizi mawili ya kikatili ya anga yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni katika mji huo, likiwemo lile lililosababisha vifo vya Wapalestina 93 baada ya jengo la makazi la familia ya Abu Al-Nasr kushambuliwa kwa bomu wakati wa asubuhi.

Jeshi la utawala ghasibu wa Israel limeendeleza mashambulizi makali kaskazini mwa Ghaza tangu Oktoba 5 kwa madai ya kuwazuia wapiganaji wa harakati ya Muqawama wa Palestina ya Hamas kujipanga upya huku likiuwekea mzingiro mkubwa eneo hilo. Hata hivyo Wapalestina wanasema, lengo la utawala wa Kizayuni ni kulipora eneo hilo na kuwahamisha wakazi wake kwa nguvu.

Zaidi ya Wapalestina 43,163 wameuawa shahidi tangu jeshi la utawala haramu wa Israel lilipoanzisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza Oktoba mwaka jana, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na zaidi ya wengine 101,510 wamejeruhiwa.

Mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayunil yamewafanya karibu wakazi wote wa Ghaza kuwa wakimbizi kutokana na mzingiro unaoendelea ambao umesababisha uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa…/