Mashambulio makali ya makombora ya Hizbullah kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel)

Leo Jumatano alfajiri vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimetangaza mashambulizi ya makombora kutoka kusini mwa Lebanon katika mji wa Safad ulioko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) na miji inayoizunguka.

Inasemekana kuwa makombora 50 yamevurumishwa katika mji wa Safad katika shambulio hilo la harakati ya Hizbullah ya Lebanon.

Kufuatia mashambulizi hayo, ving’ora  vya  hatari vya kurushwa makombora vimesikika katika maeneo hayo.

Kwa mujibu wa ripoti hii, makumi ya maelfu ya Wazayuni wamekimbilia mafichoni mapema leo alfajiri.

Kuhusiana na suala hili, jeshi la utawala katili wa  Israel lilikiri Jumanne jioni kwamba, Harakati ya  Hizbullah imerusha makombora yasiyopungua  25 kuelekea Haifa na al-Krayut inayokaliwa kwa mabavu na Israel.

Jumatatu asubuhi,  jeshi la Kizayuni lilianzisha mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Lebanon, ambayo yangali  yanaendelea hadi sasa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Afya ya Lebanon, mashambulizi hayo ya kinyama yanayotekelezwa na Israel  yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 2,350 na wengine 10,906 kujeruhiwa.

Hizbullah ya Lebanon haijakaa kimya mbele ya jinai hizo za kinyama za utawala katili wa Israel za  kuwalenga raia wa nchi hiyo. Kuanzia dakika za mwanzo kabisa, Hizbullah imekuwa ikitekeleza operesheni kali za kijeshi dhidi ya kambi za kijeshi na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika eneo la Kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ambapo katika siku na saa zilizopita, imevurumisha mamia ya makombora katika vituo vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni.