Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Masauni ametaja changamoto nne mtambuka zinazochangia Taifa kutonufaika ipasavyo na rasilimali za uchumi wa bluu ikiwemo kukosekana kwa ujuzi wa matumizi ya rasilimali za uchumi huo.
Changamoto nyingine ni kukosekana kwa mpango wa matumizi wa maeneo ya maji, uwekezaji usio wa kimkakati na fungamanishi katika matumizi ya rasilimali za uchumi wa buluu na uhaba wa utafiti na ujuzi katika matumizi ya rasilimali za uchumi wa buluu.
Nyingine ni kukosekana kwa mfumo jumuishi wa kitaasisi wa uratibu wa shughuli za uchumi wa bluu.
Masauni amesema hayo katika mkutano wa mawaziri wa kuwasilisha mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli za uchumi wa bluu nchini kwa mwaka 2024/25 na 2025/26.
Mkutano huo ulitanguliwa na kikao cha makatibu wakuu kutoka sekta zenye mnasaba na masuala ya uchumi wa buluu walikutana kwa lengo la kupitishwa, kutoa maoni, maelekezo na miongozo ya kuboresha Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu kwa mwaka 2024/25 na 2025/26 kwa lengo la kuwezesha mpango kazi husika kuwa tayari kwa ajili ya kuwasilisha mawaziri.
Akizungumzia jambo hilo, Masauni amesema kwa Tanzania, uchumi wa bluu unajumuisha shughuli za kiuchumi zilizo endelevu zinazohusiana na bahari, maziwa, mito, mabwawa, maeneo oevu na maji chini ya ardhi kwa manufaa ya jamii bila kuathiri mazingira.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamadi Masauni (katikati) akimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja (aliyesimama) wakati wa kikao cha Mawaziri cha kuwasilisha mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli za Uchumi wa Buluu nchini kwa mwaka 2024/25 na 2025/26 kilichofanyika Dodoma jana Februari 13, 2025. Wa kwanza kushoto ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari.
Amesema dhana ya uchumi wa buluu ina umuhimu mkubwa kwa Tanzania kutokana na wingi wa rasilimali zilizopo katika maji bahari na maji baridi zinazojumuisha kilomita 1,424 za ufukwe wa pwani; kilomita 700 za misitu ya mwambao; kilomita za mraba 1,440 za misitu ya mikoko; kilomita 3,560 za matumbawe; aina mbalimbali za samaki na viumbe maji wengine; takribani futi za ujazo trilioni 47.13 za nishati ya gesi asilia baharini.
Pia, amesema bandari 972 (rasmi 86 na zisizo rasmi 886); na eneo la hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Uwepo wa rasilimali hizi unachangia katika ukuaji wa uchumi katika nchi hii kupitia matumizi endelevu ya rasilimali husika.
Shughuli za uchumi wa buluu hapa nchini zinatekelezwa kwa sera, sheria, miongozo, mikakati na mipango ya kisekta ikiwemo: uvuvi, nishati, uchukuzi, maliasili na utalii, maji, umwagiliaji, viwanda na biashara, uhifadhi wa mazingira, madini, na uwekezaji.
“Mpango kazi huu wa Utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Buluu kwa mwaka 2024/25 na 2025/26 unaweka mwelekeo na msingi imara wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazowezesha Tanzania kunufaika ipasavyo na rasilimali za maji bahari na baridi,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji amesema lengo ni kunufaika na rasilimali zilizopo na alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha mwelekeo wa nini kifanyike katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa mwaka 2023, sekta ya uvuvi imeendelea kukua na kutoa mchango mkubwa katika ajira na usalama wa chakula, uzalishaji wa mazao ya uvuvi unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 473,592 hadi tani 639,092, sawa na ongezeko la asilimia 34.9 kwa mwaka 2024.