
MSHAMBULIAJI wa Kimataifa wa Tanzania, Aisha Masaka anayekipiga katika timu ya Brighton & Hove Albion ya Ligi Kuu ya Wanawake ya England, ameanza rasmi mazoezi ya uwanjani baada ya kuwa nje kwa takribani miezi mitatu.
Masaka alipata jeraha la bega kwenye mchezo wa Ligi Kuu England (W) dhidi ya Arsenal Novemba 9 mwaka jana chama lake likitandikwa jumla ya mabao 5-0.
Taarifa kutoka kwenye klabu hiyo ilieleza kuwa nyota huyo Mtanzania atarejea uwanjani mwishoni mwa Februari akiuwahi mchezo kati ya Brighton na Chelsea utakaopigwa Machi 02.
Kupitia mtandao wa Instagram wa timu hiyo imeonyesha nyota huyo maendeleo yake ni mazuri kwani tayari ameanza mazoezi ya uwanjani.
“Njia ya kupona inaendelea,” waliandika Brighton wakiambatanisha na picha ya Masaka akifanya mazoezi binafsi ya uwanjani.
Akiwa Mtanzania pekee anayecheza Ligi kubwa ya England, Masaka, staa huyo wa zamani ya Yanga Princess, amecheza dakika 10 tangu ajiunge na Brighton, dakika tatu dhidi ya Arsenal ambapo hakumaliza baada ya kuumia na dhidi ya Birmingham kwa dakika saba.