Marufuku kutumia simu vituo vya kupigia kura Uchaguzi Mkuu

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepiga marufuku matumizi ya simu za mkononi na vifaa vingine vya mawasiliano ndani ya vituo vya kupigia, kuhesabia na kujumlishia kura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025, Tangazo la Serikali Na. 249, matumizi ya simu vituoni yameruhusiwa kwa watendaji wachache wa uchaguzi tu, wakiwemo wasimamizi wa uchaguzi, wasaidizi wao na walinzi wa vituo, na hata hivyo, vifaa hivyo vinapaswa kuwa katika hali ya mtetemo (vibration) na visizalishe sauti yoyote.

“Tume imeweka masharti haya kwa lengo la kulinda utulivu, usalama na usiri wa mchakato wa uchaguzi,” imeeleza sehemu ya kanuni hizo.

Marufuku hiyo inalenga kuzuia usambazaji wa taarifa potofu, upigaji picha usioidhinishwa na vitendo vinavyoweza kuathiri mchakato wa upigaji au kuhesabu kura.

Vyama 18 vya siasa vyenye usajili kamili, Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi walisaini Kanuni hizi za Maadili. Hata hivyo, chama cha Chadema hakikusaini kanuni hizo.

Vyama 18 ndivyo vilivyosaini  kanuni hizo ambavyo ni  AAFP, ACT Wazalendo, ADA-Tadea, ADC, CCK, CCM, Chaumma, CUF, Demokrasia Makini, NLD, NRA, SAU, TLP, UDP, UMD na UPDP.

Rushwa na fujo

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeweka marufuku dhidi ya vitendo vya rushwa, fujo, lugha za matusi na udanganyifu wakati wa uchaguzi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 249, viongozi wa vyama vya siasa, wagombea, wanachama na wafuasi wao hawaruhusiwi kujihusisha na vitendo vya kuwahamasisha wapiga kura kupiga kura zaidi ya mara moja, kununua au kukusanya kadi za wapiga kura, kuharibu kura au kutoa hongo na zawadi kwa lengo la kushawishi wapiga kura au maofisa wa uchaguzi.

INEC imeeleza kuwa vitendo vya kununua kura kwa njia ya fedha au vifaa, kutoa shukrani au aina yoyote ya malipo kabla, wakati au baada ya kupiga kura ni kinyume cha sheria na vitachukuliwa hatua.

Aidha, viongozi wa vyama na wafuasi wao wametakiwa kujiepusha na matumizi ya lugha ya matusi dhidi ya maofisa wa uchaguzi, sambamba na kuvamia au kukaa kwa nguvu katika vituo vya kupigia, kuhesabia au kujumlishia kura.

Katika kanuni hizo, imeelezwa pia kuwa hairuhusiwi mtu yeyote kuhamasisha au kuwazuia wapiga kura kujitokeza siku ya kupiga kura, hatua ambayo inaweza kuathiri ushiriki wa wananchi katika mchakato wa kidemokrasia.

INEC imesisitiza kuwa lengo la masharti hayo ni kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, haki na kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia. Tume imewataka wadau wote wa uchaguzi kushiriki kwa uadilifu ili kuimarisha imani ya wananchi katika mfumo wa uchaguzi nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *