
London, England. Bao pekee lililofungwa na beki wa Manchester United, Lisandro Martinez limetosha kuipa ushindi timu hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu England (EPL) uliochezwa jana kwenye uwanja wa Craven Cottage dhidi ya Fulham.
Martinez (27) alifunga bao hilo katika dakika ya 78 kwa shuti kali lililozama moja kwa moja kwenye nyavu za Fulham.
Muargentina huyo sasa amehusika katika mabao matatu akifunga mawili na kutoa pasi moja ya bao.
Meneja, Ruben Amorim ameiongoza United katika mechi 12 za Ligi Kuu England akishinda mechi nne, ikitoka sare mbili na kupoteza mechi sita tangu alipotua ndani ya Old Trafford, Novemba 2024.
Baada ya ushindi dhidi ya Fulham, Man United imesogea hadi nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 29 katika michezo 23 ambapo imeshinda michezo nane, imepoteza michezo 10, na imepata sare katika mechi tano.
Amorim baada ya mechi kumalizika amesema timu yake inahitaji maboresho zaidi licha ya kupata ushindi huo.
“Haikuwa mechi nzuri. Tulijaribu kucheza vizuri lakini tunahitaji maboresho zaidi. Tunahitaji kuboresha namna ya kumiliki mpira. Tunapaswa kumiliki mpira zaidi na kuunda nafasi nyingi zaidi.
“Tunapata changamoto kubwa katika umiliki wa mpira, lakini kushinda kunasaidia sana.” Amesema Amorim.
Michezo mingine iliyochezwa jana ilishuhudiwa Tottenham ikifungwa mabao 2-1 nyumbani na Leicester City.
Licha ya Spurs kwenda kifua mbele kipindi cha kwanza haikuwazuia vijana wa Ruud Van Nesterlooy kupindua meza kipindi cha pili.
Tottenham imeshindwa kupata ushindi katika michezo saba zilizopita ndani ya Ligi Kuu England ikiwa imepoteza mechi sita na kupata sare mechi moja huku ikishika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 24 katika michezo 23 iliyocheza.
Matokeo ya mechi zilizochezwa jana EPL
Crystal Palace 1-2 Brentford
Tottenham 1-2 Leicester City
Aston Villa 1-1 West Ham
Fulham 0-1 Man Utd