Dar es Salaam. Mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za Injili nchini , Martha Mwaipaja, mbali na kukabiliwa na shutuma baada ya dadake, Beatrice Mwaipaja, kumshutumu kwa kutoijali familia yao licha ya mafanikio yake, sasa afichua siri ya maisha yake.
Martha amefichua siri nyuma ya maisha yake, baada ya kuzungumza na Mwananchi hivi karibuni maeneo ya Mlimani City ambapo alisema, kuna siri kubwa juu ya maisha yake ambayo wengi hawaijui.

“Watu wengi wanajiuliza, nimewezaje kuwa kwenye umaarufu wa kipaji changu cha kuimba nyimbo za Injili kwa miaka yote hiyo 13 tangu anza kuingia studio na kutoa wimbo wangu wa kwanza ‘Usikate tamaa’ mwaka 2013.
“Yapo mambo mengi, lakini kubwa ni kutokata tamaa. Mimi nikisema ninataka kitu changu, lazima kifanikiwe, huwa sikati tamaa. Kila ninapoanguka huwa ninasimama kisha ninajifuta na kusonga mbele
“Najua mimi nina roho nzuri sana. Sijawahi kuua mtu, sijawahi kudhulumu mtu, nimeshasaidia watu wengi na wala sijawahi kusema vibaya. Kuanguka ni mambo ya kawaida tu kwani na mimi ni binadamu.
“Jambo lingine ni kwamba kile kidogo ninachopata huwa ninapenda kushea na wengine na huwa mimi ninapenda sana watu, ndiyo maana nao wananipenda na imani hiyo. Kila kona nitakapopita nina watu wananipenda na mimi ninawapenda bila kujali ni watu wa aina gani. Watu wote mimi ni mashabiki wangu.

“Siri nyingine ni kwamba ninapenda sana ninachokifanya. Jamani napenda kazi yangu ya muziki, yaani ni Mungu tu anajua. sababu ninapenda ninachokifanya. Ni kitu ambacho nitadumu nacho hadi ninazeeka. Kwa hiyo wanaodhani nitakata tamaa na kuacha kuimba watangoja sana kwani kipaji changu nitadumu nacho,” alisema

Martha alipoulizwa kuhusu sakata linaloendelea mitandaoni kuhusu tuhuma za familia yake, ambapo hakutaka kuzungumzia hayo na kusema apewe muda.
“Hapana hapana, kuhusu hizo habari za familia yangu, sitaweza kuzungumza kwasasa kwani naomba nipewe muda tu,Mungu atazungumza kila kitu juu ya hili”alisema Martha