Marmoush awasha moto England

Manchester, England. Nyota wa Manchester City, Omar Marmoush jana alionyesha kwanini alisajiliwa klabuni hapo ikiwa ni baada ya kuisaidia timu yake kupata ushindi mnono dhidi ya Newcastle United katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa kwenye Uwanja wa Etihad.

Marmoush ambaye alisajiliwa dirisha dogo la usajili akitokea Frankfurt ya Ujerumani alifunga mabao matatu yaani ‘hat trick’ katika ushindi wa mabao 4-0, ilioupata Man City.

Bao la kwanza alifunga katika dakika ya 18 ambapo kipa wa City, Ederson alipiga mpira mrefu uliomkuta staa huyo ambaye alifanya kazi ya kupasia nyavuni.

Baada ya kutoa pasi ya bao la kwanza Ederson anakuwa golikipa wa kwanza kutoa asisti nyingi kwenye Ligi Kuu England akiwa mpaka sasa ameshapika mara sita.

Dakika ya 24, Marmoush alifunga bao la pili akimalizia pasi ya Gündoğan kwa kupiga shuti ambalo lilimshinda kipa wa Newcastle, Martin Dúbravka.

Dakika nane baadaye, staa huyo ambaye ni raia wa Misri alirudi tena wavuni akifunga bao la tatu baada ya kumalizia krosi ya Savinho huku akifunga mabao yote matatu ndani ya dakika 14 pekee.

Bao la nne la City lilifungwa na James McAtee katika dakika ya 84, ambaye alimalizia mpira uliopigwa na Erling Haaland.

Mpaka dakika 90, zinamalizika City iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 ikipanda mpaka nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi ikifikisha pointi 44 ikiziacha Chelsea na Bournemouth zenye pointi 43, huku ikiwa nyuma kwa pointi 13 dhidi ya vinara wa Ligi Liverpool.

Matokeo ya michezo mingine iliyochezwa jana EPL:

Leicester City 0-2 Arsenal

Aston Villa 1-1 Ipswich Town

Fulham 2-1 Nottingham Forest

Southampton 1-3 Bournemouth

West Ham 0-1 Brentford