Marioo, Rayvanny na vita ya mapenzi!

Dar es Salaam. Ingawa haizungumzwi sana kama ilivyo kwa Alikiba na Diamond Platnumz, ila unapaswa kujua kuwa kuna mpambano mkali sana tena wa chini kwa chini kati ya mastaa wawili wa Bongofleva, Marioo na Rayvanny.  

Mpambano huu hauzungumzwi sana pengine labda hauonekani na wengi kutokana na umejikita katika eneo moja dogo, nalo ni mapenzi yanayoiendesha hii dunia kama alivyoimba Alikiba katika wimbo wake, Mapenzi Yana Run Dunia (2011).

Katikati ya mpambano huu kuna watu wawili muhimu sana, Paula ambaye ni mpenzi wa Marioo na mzazi mwenziye, pia kuna Fahyma, mpenzi wa Rayvanny na mzazi mwenziye. Wawili hao kwa sehemu ndio wanaamua mchezo uende vipi. Ipo hivi.  

Ukitazama video (visualiser) ya wimbo mpya wa Marioo, Tete (2025) ambayo imetoka wiki hii, utamuona Paula, hajatokea katika video hiyo kwa bahati mbaya bali ni mpango wa makusudi ambao upo kwa muda mrefu na utaendelea kuwepo hadi lengo litimie.

Kwa ujumla hii inakuwa video ya sita yake Marioo ambayo Paula katokeo baada ya kufanya hivyo hapo awali katika video za nyimbo kama Lonely (2023), Tomorrow (2023), Sing (2023), Hakuna Matata (2024) na Unachekesha (2024).

Hivyo kwa matokeo hayo, wawili hao wameifikia rekodi ya Rayvanny na Fahyma, hivyo bado tu kuisambaratisha ingawa kwa nje lengo linaonekana ni sababu za kibiashara lakini ndani yake kuna kurushana roho ile kinoma noma!.

Chanzo cha haya yote ni kwa sababu Paula aliwahi kuwa mpenzi wa Rayvanny kabla ya kuwa na Marioo, sasa kipindi cha uhusiano wao Rayvanny alimtumia Paula katika video ya wimbo wake, Wanaweweseka (2021).

Walipoachana ndipo Marioo akawa na Paula na kuanza kumtumia katika video rasmi za nyimbo zake, utamaduni ambao Rayvanny alishakuwa nao kwa miaka mingi akiwa na mpenzi wake Fahyma.

Kabla ya kuwa na Paula, Rayvanny alishamtumia Fahyma katika video zake tatu, Kwetu (2016), Natafuta Kiki (2016) na Siri (2017), baada ya kuachana na Paula na kurejea kwa Fahyma, aliendelea kumtumia na hapo ndipo ikaonekana wanashindana na Marioo.

Baada ya kurejea kwa Fahyma, Rayvanny alimtumia mrembo huyo katika video zake tatu, Forever (2023), Habibi (2023) na Mwambieni (2023) ambazo zilitoka ndani ya mwaka mmoja kitu ambacho hakuwahi kukifanya hapo awali.

Ukweli ni kwamba hasira hizi za Rayvanny zilikuja baada ya kuona Marioo anatoa tu video na Paula, hivyo akahisi kama wamemuiga au wanataka kumrusha roho ndipo naye akajibu mashambulizi hayo ila nje mashabiki wanajua ni kazi tu ya sanaa.  

Kwa ujumla Rayvanny na Fahyma wameshatoa video sita, hivyo Marioo na Paula wamebakiza video moja tu kuisambaratisha rekodi waliyokuwa wanaishikilia ambayo ni wapenzi (couple) mastaa Bongo waliofanya pamoja video nyingi zaidi.

Je, Rayvanny atakubali kuona hilo linatimia? Usishangae akaendeleza mpambano ili kuilinda rekodi yake, na kwa vile alishatangaza kuwa mwaka huu atafunga ndoa na Fahyma, hivyo ni wazi kuwa kuna video lazima itatoka.

Hata hivyo, Rayvanny, mshindi wa BET 2017 katika video hizo sita alizofanya na Paula zote ni rasmi (official) kitu ambacho ni tofauti kwa Marioo na Paula ambao kazi zao zipo katika makundi mawili kama ifuatavyo.

Video rasmi (official) walizotoa Marioo na Paula ni tatu, Lonely (2023), Tomorrow (2023) na Sing (2023), huku zile ambazo sio rasmi  (visualizer) zikiwa ni tatu pia ambazo ni Hakuna Matata (2024), Unachekesha (2024) na Tete (2025) ambayo inafanya vizuri kwa sasa.

Kingine kinachowatofautisha wawili hao katika mpambano wao, ni kwamba Fahyma hajawahi kutokea katika video ya msanii yeyote yule ila Paula kabla ya kuwa na Marioo alishatokea katika video ya Rayvanny, Wanaweweseka (2021).

Fahyma, mwanamitindo aliyeshinda tuzo kama Scream Awards (Nigeria), Starqt (Afrika Kusini), Zikomo (Zambia) na Swahili Fashion Week (Tanzania), alishasema fedha anazomlipa Rayvanny ni nyingi kiasi kwamba hawezi kutokea katika video ya msanii mwingine.

Ikumbukwe kabla ya kuingizwa katika vita hii ya mapenzi, wawili hao walikuwa na ukaribu hadi kutoa nyimbo mbili, Te Quiero (2022) wake Rayvanny, na Anisamehe (2022) kutoka katika albamu ya kwanza ya Marioo, The Kid You Know (2021) ila sasa urafiki umekufa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *