Marie Stopes yaanzisha huduma kwa wanawake wanaoelekea kukoma hedhi

Dar es Salaam. Shirika lililojikita kutoa huduma na taarifa za afya ya uzazi nchini la Marie Stopes, limeanzisha huduma rafiki kwa kila mama, wakiwamo wanaofikia ukomo wa hedhi.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Machi 5, 2025 na Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Ufuatiliaji wa shirika hilo, Ester Lubambi kwenye kongamano la maadhimisho ya siku ya mwanamke liliofanyika jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo limebeba kaulimbiu isemayo: “Upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi ni chachu ya usawa wa kijinsia.”

Amesema mwanamke anapoelekea ukomo wa  hedhi kuna changamoto hutokea zinazoweza kuathiri utendaji wake wa kazi ofisini, nyumbani na pia mahusiano yake na familia kwa ujumla.

Miongoni mwa kadhia zinazotajwa na wataalamu waliowahi kufanya mahojiano na Mwananchi ni pamoja na baadhi yao kupoteza kumbukumbu, kutopenda kushiriki tendo la ndoa au matamanio kuongezeka, kuwa na hasira na baadhi yao hupata joto kali la mwili.

Wakieleza kuwa hiyo inatokana na ubongo, misuli na hisia kuathiriwa kutokana na mabadiliko ya kichocheo cha oestrogen.

“Ni kutokana na hilo, kupitia programu hii, tunahakikisha mwanamke anapofikia hatua hiyo inampunguzia kadhia aweze kuendelea na shughuli zake kama kawaida,” amesema.

Mbali na hilo Marie Stopes pia imeishauri  Serikali kutafuta njia mbadala ya kutoa huduma za uzazi wa mpango kwa wananchi, ikiwemo kuziingiza katika bima ya afya.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marie Stopes, Patrick Kinemo akizungumza kwenye kongamano hilo amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa nchi kuwekeza katika afya kwa kuangalia njia mbadala.

“Japokuwa Serikali imeshaanza kutoa mwongozo hasa kuhusu bima, huduma za uzazi wa mpango nazo zingeingizwa humu ingeweza kusaidia,” amesema.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mkurugenzi msaidizi wa huduma za mama na mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dk Felix Bundala amesema taarifa ya shirika hilo inaonyesha mwaka 2024 wamewafikia takriban watu milioni mbili kati ya hao wanaume walikuwa asilimia mbili, idadi ambayo ni ndogo.

“Kati ya changamoto walizoainisha hapa za kushindwa kuwafikia wanaume ni pamoja na kutokuwepo mwongozo wa kuhakikisha nao wanashiriki katika huduma hiyo.

“Naomba niwaambie bado unaendelea kukamilishwa kwani upo katika michakato mbalimbali ila muda si mrefu utatoka,” amesema.