Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi na Mama Maria Nyerere, mke wa hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ni miongoni mwa waombolezaji waliohudhuria misa ya mazishi ya Padri Felician Nkwera.
Padri Nkwera (89), mwanzilishi wa kituo cha sala na maombezi cha Mama Bikira Maria (Marian Faith Healing), alifariki dunia Mei 8, 2025 katika Hospitali ya TMJ alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuzidiwa ghafla.
Maziko yanatarajiwa kufanyika leo Jumamosi Mei 17, 2025 kituoni hapo.
Mama Maria na Dk Nchimbi waliofika kituoni hapo Ubungo Riverside, Dar es Salaam kwa nyakati tofauti wamehudhuria misa kwa ajili ya kumuombea Padri Nkwera iliyoanza saa tatu asubuhi ikiongozwa na Padri Antony Mamsery, Mkuu wa Shirika la Msalaba Mtakatifu Puma, mkoani Singida.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Emmanuel Nchimbi (katika) na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro wakiwa katika Kituo cha Maombezi na Sala cha Bikira Maria kwa ajili ya misa ya kumuaga Padri Felician Nkwera.
Mbali ya kuwa kiongozi wa kiroho, Padri Nkwera alikuwa mtaalamu wa lugha ya Kiswahili na ametunga vitabu zaidi ya saba vya kufundishia lugha hiyo, kilichokuwa maarufu ni kile cha lugha ya Kiswahili kwa wanafunzi wa sekondari na vyuo.
Padri Nkwera aliwahi pia kuhudumu Kanisa Katoliki kabla ya kutengwa na uongozi wa kanisa hilo.